Tuesday, March 3, 2015

*SERIKALI YA TANZANIA YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA SERIKALI YA DENMARK

Na Magreth Kinabo, MAELEZO Dar
Serikali ya Tanzania imetia saini mkataba wa mashirikiano na Serikali ya Denmark  wenye thamani  ya dola za Marekani  milioni 100  kwa ajili ya kusaidia mpango wa awamu ya nne wa sekta ya afya(HSPS IV) kwa kipindi cha miaka mitano ili kuwezesha kila Mtanzania kupata huduma za afya kwa wakati wote.
Mkataba  huo, ambao ni msaada kutokaDenmark  ulitiwa saini jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Dk. Donald  Mbando, Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)dawati la Afya, Dk. Deo  Mtasiwa na Balozi wa nchini,Johnny Flento.
 Akizungumzia kuhusu mkataba huo, Dk. Mbando alisema utawezesha kuongeza uwezo wa upatikanaji wa huduma za afya na kushirikisha sekta binafsi.
Dk. Mbando alisema alizitaja asasi za kiraia ambazo  nazo zilitia saini mkataba huo kuwa ni Sikika, CCBRT, Mariastopers na Muungano wa hospitali binafsi. 
“Msaada huu umekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa tuko katika hatua ya  kukamilisha mpango wa awamu wa sekta ya afya wa awamu  ya tatu, hivyo utasaidia kutekeleza mpango wa awamu ya nne na Matokeo Makubwa Sasa(BRN) kwenye sekta ya afya,ambapo utaongeza  upatikanaji wa rasilimali watu, dawa na vifaa tiba,” alisema Dk. Mbando.
Aliongeza kuwa utasaidia pia kuongeza jitihada za kupunguza vifo wa watoto na wakina mamawajawazito ambavyo bado ni changamoto.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark,Flento alisema ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali ni muhimu ili kuwezesha upatikanaji wa huduma  bora za afya kwa kila mtu. Pia utasaidia  kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya afya,zikiwemo za usimamizi wa fedha za umma  na  upungufu wa rasilimali watu.
Naye Mkurugenzi wa Sikika Irenei Kiria alisema ushirikishaji wa sekta binafsi katika mkataba huo, utaongeza uwajibikaji, utoaji wa huduma za afya kwa kiwango kinachotakiwa na kuhakikisha  rasilimali zinatumika ipasavyo.

*KAMATI YA MASHINDANO YATOA UAMUZI WA KUZISHUSHA DARAJA TIMU ZA UJENZI RUKWA, VOLCAN FC

Timu za Ujenzi Rukwa na Volcano FC ya Morogoro zimeshushwa madaraja mawili hadi ligi za wilaya baada ya kushindwa kufika uwanjani kwenye mechi zao za Ligi Daraja la Pili (SDL).
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
Ujenzi Rukwa ilishindwa kwenda Kigoma kuikabili Mvuvumwa FC ya huko wakati Volcano FC haikutokea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo ilitakiwa kucheza na Wenda FC.
Uamuzi wa Kamati ya Mashindano umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 27 ya SDL ambapo mbali ya kushushwa madaraja mawili, lakini pia timu hizo zimepigwa faini ya sh. milioni moja kila moja. Vilevile matokeo yote ya mechi zao kwenye Ligi hiyo yamefutwa.
Nayo Singida United imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Ujenzi Rukwa kubainika kumchezesha mchezaji asiyestahili (non qualified) kwenye mechi iliofanyika Februari 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Mchezaji Emmanuel Elias Mseja wa Mbao FC amepigwa faini ya sh. 100,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya kukojoa uwanjani kwenye mechi dhidi ya AFC iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Pia viongozi wa Mbao FC, Abdallah Chuma (Daktari) na Meneja Yasin Abdul wamefungiwa miezi sita na faini ya sh. 100,000 kila mmoja kwa kumtukana na kumtishia maisha Kamishna wa mechi hiyo.
Nayo klabu ya AFC imepigwa faini ya sh. 300,000 kutokana na washabiki wake kuifanyia vurugu timu ya Bulyanhulu FC kwenye mechi yao iliyofanyika Februari 7 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Timu ya Magereza Iringa imepigwa faini ya jumla ya sh. 200,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na uwanjani kwenye mchezo wao na Njombe Mji uliochezwa Februari 21 mwaka huu. Naye mchezaji wa timu Amasha Mlowasa amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 100,000 kwa kumtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi hiyo.

*MVUA, UPEPO MKALI VYATIBUA MAONESHO YA SIKU YA WANAWAKE MJINI MOROGORO

  Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Bi. Theresia Muhongo akisikiliza maelezo kutoka kwa Haji Sajilo ambaye ni Kiongozi msimamizi wa Mipango wa NGO,s ya MOYODEI wakati alipotembelea kwenye mabanda yaliyoharibiwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha jana jioni. Mabanda hayo yalikuwa ni kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani iliyokuwa ianze leo jumanne lakini kutokana na maafa hayo maonyesho hayo yamesogezwa mbele hadi tarehe 5/03/2014 kwa ajili ya ukarabati wa mabanda hayo.
 Mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, Bi. Theresia Muhongo akipata maelezo kutoka kwa mama kuhusu mabanda yaliyoezuliwa na mvua iliyokuwa na upepo mkali
 
Baadhi ya Mabanda yakiwa yameharibika vibaya. Picha na Pamoja Geofrey Adroph

Monday, March 2, 2015

*MWENDELEZO WA TAARIFA KUHUSU KUKOSEKANA KWA MTANDAO WA LUKU

UPDATE ON LUKU PROBLEM MARCH 02, 2015.

SHIRIKA LA UMEME TANZANIA
(TANESCO)
MWENDELEZO WA TAARIFA KUHUSU KUKOSEKANA KWA MTANDAO WA LUKU

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kutoa mwendelezo wa taarifa ya tatizo la kukosekana kwa huduma ya kununua umeme wa LUKU kwa njia ya Mtandao lililoanza usiku wa kuamkia Februari 28, 2015.
Kama tulivyoeleza awali, Tatizo kubwa lilikuwa ni hitilafu ya kiufundi iliyotokea kwenye mfumo wa kununua umeme wa LUKU.
Baada ya kugundua tatizo, mafundi wa Tanesco na Kampuni ya Itron kutoka Afrika Kusini ambao ndio watengenezaji wa mfumo huo, wamefanikiwa kurejesha huduma ya kununua umeme wa LUKU kwa njia ya Benki. Benki za CRDB na NMB kwa kutumia simbanking na ATM kwa sasa wanaweza kuuza umeme. Pia Maxmalipo nao wameanza kuuza kwa baadhi ya vituo.
Mitandao ya simu (M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money) bado hawajaanza kuuza.  
Jana tuliwashauri wateja wetu kwenda kununua umeme kwa Mawakala wetu na baadhi walifanya hivyo lakini baadae tuligundua kuwa units (tokens) walizokuwa wametumiwa zilikuwa haziingii kwenye mita zao, hivyo tukasimamisha kununua kwa kutumia mawakala mpaka tutakapo rekebisha tatizo.
Tunawaomba Wateja wote ambao wana tokens ambazo hazikuingia kwenye mita zao wawe na subira kwani tutoa maelekezo baada tu ya mfumo kurudi kwenye hali ya kawaida.
Aidha tunawapa matumaini wateja wetu kuwa tatizo tutalipatia ufumbuzi muda si mrefu na wale wote ambao walishatuma pesa zao kwa njia ya simu na hawajapa tokens, mfumo ukitengamaa watatumiwa tokens zao. Hakuna pesa ya mteja itakayopotea.
Uongozi wa Shirika unaendelea kunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano
TANESCO Makao Makuu.

*HABARI KUTOKA TFF LEO, TFF YATUMA SALAM ZA PONGEZI FMF

Rais wa Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini –TFF Bw. Jamal Malinzi ametuma salama za pongezi kwa Rais Boubacar Diara wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Mali (FMF) kwa kutwaa Ubingwa wa Afrika kwa vijana U17.
Katika salam zake mh. Malinzi amesema mafanikio mazuri waliyoyapata  FMF yametokana na uongozi bora, kamati ya utendaji na mipango thabiti waliyoiweka katika soka la Vijana.
Kwa kutwaa Ubingwa wa vijana Afrika U17, Mali wamepata nafasi ya kuliwakilisha Bara la Afrika kwenye fainali za U17 za Dunia nchini Chile pamoja na nchi za Afrika Kusini,Guinea na Nigeria.
Mali wametwaa Ubingwa wa vijana Afrika U17 baada ya kuifunga timu ya taifa ya vijana ya Afrika Kusini (Amajimbo's) kwa mabao 2-0.
Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), watanzania wanawapa pongezi  Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Mali (FMF) wa kutwaa Ubingwa huo.
Aidha Rais Malizi pia ametuma salam za pongezi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Afrika Kusini (SAFA) Bw. Dany Jordaan kwa timu ya Amajimbo's kushika nafasi ya pili.
Amajimbo's ndio timu pekee kusini mwa Bara la Afrika watakaowaklisha kwenye fainali za U17 za Dunia nchini Chile.
*BEACH SOCCER YAENDELEA KUJIFUA BAMBA BEACH
Timu ya Taifa ya Tanzania ya Sola la Ufukweni (Beach Soccer) iliyoingia kambini mwishoni mwa wiki Bamba Beach Kigamboni, inaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya timu ya Taifa Soka la Ufukweni ya Misri mwishoni wiki ijayo.
Maandalizi ya mchezo dhidi ya timu ya Misri yanaendelea vizuri Bamba Beach Kigamboni chini ya kocha mkuu John Mwansasu ambaye aliingia kambini mwishoni mwa wiki na wachezaji 14.
Mchezo wa kwanza unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya Machi 13 katika klabu ya Escape 1 Msasani jijini  Dar es salaam na marudio yake kufanyika baada ya wiki moja nchini Misri.
Tanzania ilifanikiwa kufuzu hatu ya pili baada ya kuitoa timu ya Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12- 9, mchezo wa awali Mombasa Tanzania ilishinda kwa mabao 5-3, na mchezo wa marudiano uliofanyika klabu ya Escape 1 kuibuka na ushindi wa mabao 7-6.
Fainali za Mataifa Afrika kwa Sola la Ufukweni (Beach Soccer) zinatarajiwa kufanyika mwezi April 2015 katika Visiwa vya Shelisheli.
*VPL KUENDELEA JUMATANO
Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea kutimua vumbi katika viwanja vitatu tofauti siku ya jumatano, Mkoani Morogoro katika uwanja wa Manungu-Turiani timu ya Mtibwa Sugar watawaribisha majirani zao timu ya Polisi Morogoro.
Katika uwanja wa Azam Complex - Chamazi maafande wa JKT Ruvu watawakaribisha maafande wenzao timu ya Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya, huku timu ya Ruvu Shooting wakiwa katika Uwanja wa nyumbani Mabatini - Mlandizi kuwakaribisha timu ya Ndanda FC.

*MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AAGANA NA BALOZI WA JAPAN ALIYEMALIZA MUDA WAKE, MASAKI OKADA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada, wakati akimkaribisha Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Machi 2, 2015. Balozi Okada alifika ofisini kwa Makamu kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo, kwa ajili ya mazungumzo na kumuaga rasmi baada kumaliza muda wake wa kazi nchini. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja ya kumbukumbu na Balozi wa Japan nchini Tanzania, aliyemaliza muda wake wa kazi, Masaki Okada, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam. 

*BONDIA IBRAHIMU CLASS 'KING CLASS MAWE' ANYAKUWA UBINGWA WA U.B.O AFRICA KWA KUMTWANGA COSMAS CHEKA

Bondia Ibrahimu Class 'King Class Mawe' (kushoto) akichapana na Cosmas Cheka wakati wa pambano lao la kuwania ubingwa wa U.B.O Africa, lililofanyika  mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Uwanja wa ndani wa Taifa. Katika pambano hilo King Class alishinda kwa pointi na kutwaa mkanda huo ambapo kwa sasa Class anashikilia mikanda miwili ya ubingwa wa Africa W.P.B.F na U.B.O Africa.
Bondia Ibrahimu Class 'King Class Mawe' askiwa na mikanda yake ya ubingwa wa Africa wa U.B.O na WPBF, baada ya kutangazwa mshindi.
Bondia Ibrahimu Class 'King Class Mawe' akishangilia ushindi na mashabiki wake baada ya kutangazwa mshindi kwenye pambano lake na Cosmas Cheka.
 Bondia Francis Miyeyusho (kushoto) akikwepa konde la Fadhil Majiha, wakati wa pambano lao la raundi nane. Katika pambano hilo Majiha alishinda kwa Pointi.
  Bondia Francis Miyeyusho (kushoto) akikwepa konde la Fadhil Majiha, wakati wa pambano lao la raundi nane. Katika pambano hilo Majiha alishinda kwa Pointi.
 Ilikuwa ni patashika, pambano hili la Miyeyusho na Majiha......
Miyeyusho akimpeleka chini Majiha.


*RAIS JK, MAKAMU WAKE DKT. BILAL WAWAONGOZA WANANCHI KUAGA MWILI WA MAREHEMU KAPTENI KOMBA KARIMJEE DAR

 Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete, wakitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili wa marehemu Kapteni John Komba, wakati wa shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, leo mchana. Baada ya shughuli hiyo ya kuaga mwili huo ulisafirishwa kuelekea Jiji cha Litui, Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma kwa maziko, yanayotarajia kufanyika kesho. Leo jioni katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea pia kutakuwa na shughuli ya kuaga mwili huo ambapo wakazi wa Mkoa huo watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakeze Mama Zakhia Bilal na Mama Asha Bilal, wakitoa heshima zao za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa marehemu, Kapteni John Komba, wakati wa shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika leo, kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Baada ya shughuli hiyo mwili wa marehemu umesafirishwa kuelekea Kijiji cha Litui Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kwa maziko.
 Wanafamilia wakiwasili kwenye viwanja hivyo...
 Mke wa marehemu Kapteni Komba, Mama Salome Komba, akiwasili kwenye viwanja hivyo.
 Wapambe wa Bunge la Jamhuri, wakibeba Jeneza lenye mwili wa marehemu wakati likiwasili kwenye viwanja hivyo.
 Jeneza hilo likiwa katika viwanja hivyo.
 Baadhi ya viongozi waliohudhuria shughuli hiyo kwenye viwanja vya Karimjee.
 Baadhi ya viongozi waliohudhuria shughuli hiyo kwenye viwanja vya Karimjee.
 Baadhi ya viongozi waliohudhuria shughuli hiyo kwenye viwanja vya Karimjee.
 Mwakilishi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Joshua Nassari, akizungumza kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya upinzani.
 Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, akizungumza kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya CCM.
 Spika wa Bunge la Jamhuri, Mhe. Anne Makinda, akizungumza kwa niaba ya wabunge.
 Mwandishi wa habari wa Uhuru, Mariam, akionekana kubugujikwa na machozi wakati wasanii wakiimba jukwaani.
 Msanii Lubi akiimba wimbo maalumu jukwaani.
 Wasanii wa muziki wa dansi wakiimba wimbo maalum jukwaani.
 Wasanii wa Bongo Flava na Bongo Movie wakiimba wimbo maalum jukwaani.
 Makamu wa Rais, Dkt. Bilal, akiagana na Spika wa Bunge Mstaafu, Pius Msekwa wakati akiondoka kwenye viwanja hivyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, wakati walipokutana kwenye Viwanja vya Karimjee baada ya kuhudhuria shughuli za kuaga mwili wa marehemu Kapteni John Komba leo. Baada ya shughuli hiyo mwili wa marehemu umesafirishwa kuelekea Jijini cha Litui Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kwa maziko. 

*SHUGHULI YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU KOMBA MUDA HUU VIWANJA VYA KARIMJEE MUDA HUU

Shughuli za kuagwa mwili wa marehemu Kapteni Damian Komba, zinaendelea kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, muda huu.

Sunday, March 1, 2015

*KIFO CHA KAPTENI JOHN KOMBA CHAISHITUA CCM, AACHA AMEREKODI WIMBO MMOJA TU WA KAMPENI 2015

Kapteni John Komba, (pichani chini) enzi za uhai wake akiwa nyumbani kwake katika moja ya harakati za kuandaa nyimbo za Kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015.

Marehemu Kapteni John Komba, alikuwa tayari ameanza kufanya mazoezi ya kurekodi albam ya  nyimbo za uchaguzi mkuu wa 2015 za Chama cha Mapinduzi CCM, ambapo alikuwa akishirikiana na baadhi ya wanamuziki wake wa zamani aliokuwa nao katika bendi ya TOT kuandaa nyimbo hizo kabla ya kupeleka kwa kundi zima ili kufanyia mazoezi na kurekodi baada ya kupitishwa.

Wanamuziki hao ni pamoja na Thabit Abdul, aliyekuwa akipiga gitaa la besi na Kinanda, Jerry Juma almaarufu kama JJ, ambaye pia alikuwa akipiga Kinanda, Korobiniani Mkinga, na Gaspar Tumaini.

Akizungumza na mtandao huu mmoja wa wanamuziki hao, Jerry Juma almaarufu kama 'JJ Mzee wa Mbezi', alisema kuwa Marehemu alikuwa amewaalika kushiriki katika kuandaa nyimbo hizo na tayari walikuwa wakifanya mazoezi nyumbani kwake pale Tangibovu Mbezi Beach.

Aidha Jj, alisema kuwa hivi majuzi siku ya Ijumaa kabla ya kifo chake walikuwa pamoja usiku wakifanya mazoezi, ndipo alipowaambia kuwa alikuwa hajisikii vizuri hivyo akaomba apumzike na wamuachie kazi ya kuandika na akawaahidi kuwa akipata nafuu ataamka usiku ili aanze kuandika mashahiri ya nyimbo hizo walizokuwa wakifanyia mazoezi na kuwataka wakutane Jumapili kwa ajili ya kupitia alipofikia ili kufanya marekebisho.

''Tulikuwa tukifanya mazoezi pale nyumbani kwake ghafla, akaanza kusema kuwa hajisikii vizuri, akaomba feni ikaanza kumpepea huku akiendelea nasi kufanya mazoezi, lakini baada ya muda akasema kuwa hajisikii vizuri anahisi kuzidiwa na ndipo alipotuomba kusitisha ili akapumzike na akatuahidi kuwa akipata nafuu ataamka usiku ili aanze kuandika ili kesho yake amalizie kurekebisha ili tukutane siku ya Jumapili tuendelee na mazoezi, lakini kwa bahati mbaya siku iliyofuata Jumamosi akafariki dunia ni kazi ya Mungu''. alisema Jj

Katika Albam hiyo iliyotakiwa kuwa na jumla ya nyimbo tano walishafanikiwa kurekodi wimbo mmoja uitwao CCM Mbele kwa Mbele, ambao waliutumia katika sherehe za miaka 38 ya CCM zilizofanyika kitaifa Mkoani Ruvuma Songea mwezi uliopita.

Wimbo wa pili waliokuwa wakifanyia mazoezi kabla ya kifo cha Kiongozi wao Kapten Komba, unaitwa, Kimewaka kwa CCM Kimenuka kwa Wapinzani, ambao kwa asilimia kubwa ulikuwa ukielekea kukamilika iwapo wangefanikiwa kukutana siku ya Jumapili kama si kofo hicho ili kuongezea maneno na kufanya marekebisho machache kabla ya kufikisha kwa kundi kufanyia mazoezi na kisha kurekodiwa.

Aidha JJ, alisema kuwa katika ablam hiyo alikuwa tayari ametunga wimbo wake mmoja uitwao Wapinzani wamekula za Chembe Lazima wakae, ambao tayari ulikwisha pitishwa na Kiongozi wao marehemu Komba, ambaye alishasema kuwa katika Wimbo huo haongezi wala hapunguzi neno bali ni kufanyia mazoezi tu.

''Ni kweli CCM imepata pengo kubwa sana kwa kuondokewa na Kiongozi wetu Kaapteni John Komba, lakini tunawaahidi Viongozi wetu wasihofu kwani Msiba huu ni wetu sote na Komba ameacha Hazina kubwa ya Vipaji ambayo itafanya yote yaliyoachwa na Kapteni Komba na kwa uhakika ili kumuenzi kiongozi wetu huyu''. alisema JJ

Wimbo huo uliorekodiwa ulifanyiwa kazi katika Studio za Hiland zilizopo Kigogo jijini dar es Salaam, chini ya mwandaaji, Rich, ambapo pia na hizo zilizobaki zinatarajia kuandaliwa katika studio hiyo.

ambapo walitakiwa kuingia studio kurekodi wimbo wa pili wiki hii, lakini kwa mapenzi ya mungu Kiongozi huyo ameacha kazi hiyo bila kuimalizia na kuacha majonzi makubwa kwa wana CCM na Watanzania kwa ujumla.

Marehemu Komba (katikati) akiwa na kundi lake la TOT katika moja ya shughuli za CCM.

*RAIS WA ZANZIBAR DKT. SHEIN ASHIRIKI HITMA YA MEREHEMU SALIMIN AWADH

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akijumuikana Viongozi na waislamu katika kisomo cha Hitma ya Marehemu Salmin Awadh aliyekuwa Mwakilishiwa Jimbo la Magomeni (CCM) iliyosomwa leo jioni katika Msikiti wa Mushawal Mwembeshauri Mjini Unguja hitma hiyo ilihudhuriwa na Waumini na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi.
 Baadhiya Waislamu na Viongozi mbali mbali na wananchi wakiwa katika kisomo cha Hitma ya kumuombea Dua Marehemu Salmin Awadh aliyekuwa Mwakilichi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Mjini Unguja aliyefariki hivi karibuni Hitma hiyo ilisomwa leo jioni katika Msikiti wa Mushawal Mwembeshauri.
 Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akitoa mawaidha baada ya kisomo cha Hitma ya Marehemu Salmin Awadh aliyekuwa Mwakilichi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Mjini Unguja aliyefariki hivi karibuni Hitma hiyo ilisomwa leo jioni katika Msikiti wa Mushawal Mwembeshauri.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai akitoa shukurani kwa Viongozi mbali mbali Waislamu na Wananchi na wapenzi wa CCM baada ya kisomo cha Hitma Marehemu Salmin Awadh aliyekuwa Mwakilichi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Mjini Unguja iliyosomwa leo katika Msikiti wa Mushawal Mwembesahauri Marehemu alifariki hivi karibuni na kuzikwa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na IKULU

*TASWA KUSHIRIKI MKUTANO WA 78 WA CHAMA CHA KIMATAIAFA CHA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatarajia kushiriki kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) unaotarajiwa kuanza kesho (Jumatatu) Paris, Ufaransa.
TASWA katika mkutano huo itawakilishwa na Mwenyekiti wa chama, Juma Pinto na Katibu Mkuu, Amir Mhando ambao wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo (Jumapili) alasiri kwa ndege ya Emirates wakipitia Dubai.

Mkutano huo wa kawaida wa mwaka ambao utamalizika Machi 4, 2015 utashirikisha viongozi wa zaidi ya vyama vya waandishi wa habari za michezo 150 duniani, utaambatana na mijadala pamoja na semina mbalimbali kuhusiana na uandishi wa habari za michezo.
Pia kutatolewa taarifa kuhusiana na maandalizi ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2016 Rio de Jainero, Brazil, ambapo mhusika mkuu atakuwa Mkuu wa Masuala ya Habari wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Anthony Edgar.
Baadhi ya mada zingine katika mkutano huo zitatolewa na wawakilishi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).Pia kutakuwa na uwasilishaji wa mada kwa vyama mbalimbali vya kimataifa vya michezo.
Pia washiriki watapata mafunzo ya changamoto zinazokabili uandishi wa habari za michezo kutokana na kuenea haraka kwa mitandao ya kijamii.

TASWA inalishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kampuni ya Jambo Concepts inayochapisha gazeti la JamboLeo kwa kugharamia tiketi za ujumbe huo.
 TASWA ni mwanachama hai wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS) chenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi, ndiyo sababu kila mwaka tumekuwa tukishiriki mikutano hiyo.

*RATIBA YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU KAPTEN KOMBA LEO KARIMJEE

NA.
MUDA
TUKIO
MHUSIKA

1.
12:00 - 01:00

Familia na Waombolezaji kupata chai nyumbani

Kaimu Katibu wa Bunge
2.
01:00 - 04:00
Misa ya kuaga mwili wa Marehemu

Kanisa Katoliki,
Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa

3.
04:00 - 04:30
·         Ndugu, Jamaa na Wananchi kuwasili katika Viwanja vya Karimjee

·         Viongozi wa Vyama vya Siasa, Waheshimiwa Wabunge, Manaibu Waziri, Mawaziri kuwasili na kuketi katika nafasi zao

Katibu wa Bunge

4.
04:33
Kiongozi wa Upinzani Bungeni  kuwasili

Kaimu Katibu wa Bunge
5.
04:36
Mhe. Naibu Spika kuwasili

Kaimu Katibu wa Bunge
6.
04:39
Mhe. Spika kuwasili

Mhe. Naibu Spika
7.
04:42
Mhe. Waziri Mkuu kuwasili

Mhe. Spika
8.
04:50
Mhe. Makamu wa Rais kuwasili
Mhe. Spika

9.
05:00
Mhe. Rais kuwasili

Mhe. Spika
10.
05:00
Mwili wa Marehemu kuwasili  kwa gwaride maalum la Sergeant-At-Arms

Katibu wa Bunge
11.
05:00 - 05:15
Sala fupi
Kanisa Katoliki,
Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa
12.
05:15 - 05:20
Wasifu wa Marehemu

Kaimu Katibu wa Bunge
13.
05:20 - 05:30
Salamu na Rambirambi za Chama cha Mapinduzi (CCM)

Katibu Mkuu, CCM
14.
05:30 - 05:35
Salamu na Rambirambi kutoka kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni

Kiongozi wa Upinzani Bungeni
15.
05:35 - 05:45
Salamu na Rambirambi za Serikali

Waziri Mkuu
16.
05:45 - 05:55
Salamu na Rambirambi za Uongozi wa Bunge

Mhe. Spika
17.
05:55 - 06:00
Neno la Shukrani toka kwa familia

Mwakilishi wa Familia
18.
06:00 - 06:15
Utaratibu wa safari

Kaimu Katibu wa Bunge
19.
06:15 - 07:15
Kuaga Mwili wa Marehemu kulingana na Itifaki

MC
20.
07:15
Mwili wa Marehemu kuondoka uwanjani kuelekea Uwanja wa Ndege

MC
21.
07:20 - 07:25
Viongozi wa Kitaifa kuondoka kulingana na Itifaki

MC
22.
07:40
Mwili wa Marehemu kuwasili Uwanja wa Ndege

Kaimu Katibu wa Bunge
23.
08:00
Mwili, Familia na Waombolezaji kuondoka kuelekea Songea

Kaimu Katibu wa Bunge
24.
10:00
Mwili wa Marehemu kuwasili Uwanja wa Ndge Songea na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
25.
10:00 - 10:15
Mwili wa Marehemu kuelekea Uwanja wa Majimaji

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
26.
10:15 - 11:00
Mkuu wa Mkoa kuongoza wakazi wa Ruvuma kuaga mwili wa Marehemu

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
27.
11:00 - 01:00
Mwili wa Marehemu kuondoka Uwanja wa Majimaji kuelekea Lituhi, Nyasa

·         Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

·         Kaimu Katibu wa Bunge
28.
01:00
Mwili kuwasili nyumbani na taratibu za kifamilia kuendelea

MC