Habari za Punde

*HASSAN KESSY AIDHINISHWA KUCHEZA YOUNG AFRICANS, SIMBA WATAKIWA KUMLIPA MISHAHARA YA MIEZI 3

Kamati ya Sheria na Haki za wachezaji imepitisha usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara huku ikiwa imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kesi’ kuitumikia Young Africans kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.

Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Young Africans kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.

Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Young Africans wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.

Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa. 
Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu Meneja wa mchezaji huyo, Athuman Tippo,  alisema kuwa anawashangaa Simba kwa kuendelea kung'ang'ania kulipwa sh. milioni 120, pamoja na kwamba mchezaji huyo tayari amekwisha idhinishwa kucheza katika Klabu yake mpya.

Aidha Tippo alisema kuwa Hassan Kessy ndiye anayetakiwa kulipwa na Simba mishahara yake ya miezi mitatu aliyoiacha kabla ya kuipa kisogo timu hiyo  na si kama wanavyodai na kuendelea kuwadanganya waandishi wa habari ukweli wa mambo.

''Hao Simba bado siwaelewi, kwani sioni mantiki ya kudai kiasi hicho cha fedha wakati tayari TFF imekwisha muidhinisha mchezaji kucheza msimu ujao baada ya kuona kuwa hana tatizo katika uhamisho wake,

Wao Simba ndiyo hasa wanatakiwa kumlipa Kessy mishahara yake ya miezi mitatu aliyoiacha walipomfungia na kuamua kusaini na Yanga, japo bado sijaletewa rasmi madai hayo na wao lakini ninachweza kushukuru ni kuruhusiwa kwa mchezaji kucheza hayo mengine haki itajulikana tu''. alisema Tippo 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.