Habari za Punde

*PANGANI YAPATA KIVUKO KIPYA

Na Theresia Mwami TEMESA

Wananchi wa Pangani na Bweni mkoani Tanga wamepata kivuko kipya cha MV. Tanga ambacho sasa kitasaidiana na MV. Pangani II kutoa huduma katika eneo la Pangani na Bweni.

Akiongea na wananchi wa Pangani mara baada ya kuzinduliwa kwa kivuko hicho Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Lekujan Manase amesema kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kipya cha MV. Tanga ni muendelezo wa sera ya Serikali ya kuboresha huduma ya vivuko katika maeneo mbalimbali yaliyo na mahitaji ya vivuko nchini.
“TEMESA imejipanga kuhakikisha kuwa vivuko vyake vyote vinafanyiwa matengenezo ya kinga kwa wakati, ili kuhakikisha kuwa huduma kwa wananchi wanaotumia vivuko hivyo inapatikana kwa wakati muafaka” Alisema Mhandisi Manase.
Mhandisi Manase ameongeza kuwa hivi sasa MV. Pangani II itakwenda kwenye ukarabati mdogo na baada ya ukarabati huo vivuko vyote viwili vitabakia katika eneo la Pangani na Bweni ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Lazaro Vazuri alisema kuwa kivuko cha.
MV. Tanga ni mwanzo wa uboreshaji wa huduma ya vivuko nchini na kwa sasa wapo katika mikakati ya kukarabati vivuko vilivyopo na kujenga vivuko vingi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vivuko katika baadhi ya maeneo.
Mmoja ya wananchi wa Pangani Bw. Othman Juma Ali ameipongeza Serikali kwa juhudi za kupambana na changamoto ya vivuko inayozikumba sehemu nyingi zilizozungukwa na maji.
“Tumekipokea kivuko cha MV. Tanga kwa furaha kubwa na tunaiomba Serikali kutoa huduma ya kivuko hiki kwa saa 24 kila siku ili kitusaidie wananchi hasa wa eneo la Bweni kupata huduma hiyo nyakati za usiku tunapohitaji kupata huduma za kijamii upande wa Pangani” alisema Bw. Othman.
MV. Tanga imesanifiwa na kutengenezwa na Kampuni ya kitanzania ya Songoro Marine Company Ltd na kivuko hiki kina uwezo wa kubeba tani 50 ambazo ni sawa na kubeba abiria 100 na magari 6 kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.