Habari za Punde

*BALOZI IDDI AUNGANA NA WANACHAMA 8,500 KUJIUNGA NA MFUKO WA KUCHANGIA KWA HIYARI ZANZIBAR

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Afisa Huduma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Fatma Abass Mohammed, pesa za kujiunga rasmi na Mfumo wa kuchangia kwa hiyari ulioanzishwa na ZSSF tokea mwaka 2012. Makabidhiano hayo yamefanyika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto ni Meneja Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar,  Khalifa Muumin Hilal.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Khalifa Muumin kushoto na Afisa Huduma wa Mfuko huo Fatma Abass Mohammed, baada ya Mhe Balozi juzana fomu za kujiunga na mfuko huo. Picha na – OMPR – ZNZ.
********************************************
Zaidi ya Watu  Elfu 8,500 wameshajiunga kuwa Wanachama wa Mfuko wa kujichangia kwa hiyari ulioanzishwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar        { ZSSF } mnamo mwaka 2012 ukiwa na lengo la kumpa hifadhi mwanachama pale ambapo hawezi kufanya kazi kutokana na majanga mbali mbali.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Nd.  Khalifa Muumin Hilal  katika hafla fupi ya kumsajili rasmi kuwa mwanachama wa Mfuko huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Usajili huo wa hiyari ambao tayari wameshafanyiwa baadhi ya Masheha, Madiwani, Wawakilishi, wajasiri amali, Wananchi wa kawaida wakiwemo pia wanafunzi amefanyiwa Balozi Seif  baada ya kuridhia kwa hiari yake hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Ndugu Khalifa Muumin Hilal alisema mpango huo unahusisha watu wa rika zote wakiwamo wanachama wa ZSSF  na wafanyakazi walio katika sekta rasmi, Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi { Diaspora }na wale ambao hawajachangia kwenye mfuko wowote wa hifadhi ya jamii kutokana na ajira zao kukotegemea kipato cha kila mwisho wa mwezi.
Meneja huyo wa Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar alifafanua kwamba  ZSSF imejipanga kumnufaisha mwananchi kwa kumpatia hifadhi na kumshajiisha kujiwekea akiba itakayomfaa kwa maisha yake ya sasa na yale ya baadaye.
Alieleza kwamba Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar unaendelea kupata faraja kutokana na kuona kwamba Viongozi walio wengi wa Taasisi mbali mbali za Umma na hata zile za binafsi wameamua kujiunga na mfuko huo.
“ Hifadhi ya Jamii lazima iende mbali zaidi katika kuona mustakabala wa maisha ya Jamii unakuwa mzuri na muelekeo sahihi unaokubalika katika mazingira bora ya kila siku ya mwanaadamu “. Alisema Ndugu Muumin.
Naye kwa upande wake akikamilisha zoezi la usajili huo wa mfuko wa kujichangia kwa Hiari Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar kwa ubunifu wake katika muelekeo wa kuona hifadhi ya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba inatengemaa.
Balozi Seif alisema juhudi za Mfuko huo katika kutoa elimu na maarifa jinsi ya umuhimu wa  mfuko huo kupitia vyombo mbali mbali vya Habari ndizo zilizomshawishi na kufikia hatua rasmi ya kujisajili na kuwa mwanachama wa mfumo huo.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } umeanzishwa kwa sheria nambari 2 ya mwaka 1998, na kufanywa maboresho kadhaa na hatimae kuanzishwa upya kwa sheria nambari 2 ya mwaka 2005.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii  Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha sheria nambari 44 {b} cha mwaka 2005, umeanzisha mfuko wa uchangiaji wa hiyari unaojuilikana kama Zanzibar Voluntary Social Security Scheme { ZVSSS }.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.