Habari za Punde

*KUELEKEZA MCHEZO WA KESHO YANGA VS SIMBA TIMU HADI MASHABIKI HOMA IMEPANDA

Na Ripota wa Sufianimafoto, Dar.
HOMA ya mechi ya watani wa Jadi baina ya Yanga na Simba inazidi kupamba moto kwa kila upande kujinadi kumsambaratisha mwenzake siku ya kesho.

Mtanange huo unapigwa kesho kwenye dimba la Uwanja wa Taifa majira ya saa 10, jioni, ukichezeshwa na Mwamuzi mwenye beji ya FIFA, Martin Sanya akisaidiwa na Frank Chacha na Mpenzu huku mezani akiwa Hery Sasii.

Katika mchezo huo Serikali imesimamia zoezi zima la utumiaji wa mfumo mpya wa kadi za kieletroniki ambao umekuwa na hamasa kubwa na changamoto nyingi kwa mashabiki wengi waliojitokeza kuchukua kadi hizo.
Yanga wakiwa njiani kuingia Dar es salaam wakitokea Pemba walipoweka kambi ya wiki moja, Simba tayari wameingia jijini na asubuhi ya leo walifanikiwa kufanya mazoezi mepesi kwenye uwanja wa Gymkhana.

Timu hizi zimeweza kukutana mara 96 na tayari Mabao 196 yakiwa yamefungwa huku katika mechi tano tano za mwisho Yanga ameshinda mara mbili, Simba ikishinda mara moja na sare mbili, huku Yanga Ikiwa haijabadilisha benchi la ufundi pamoja na kikosi kwa muda mrefu wanakutana na Simba ambayo imebadilisha asilimia kubwa ya wachezaji na benchi la ufundi.

Aidha siku ya Jumapili, michezo itakuwa mitano kati ya Mbeya City itaikaribisha Mwadui kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya; Majimaji itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati African Lyon itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Mvomero mkoani Morogoro. 

Mbao na JKT Ruvu Jmwatakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini huko Mlandizi wakati Kagera itaikaribisha Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.