Habari za Punde

*RAIS DKT. MAGUFULI AJIBU KILIO CHA MUDA MREFU CHA WAKAZI WA ZILIZOKUWA NYUMBA ZA MAGOMENI KOTA, AWAAHIDI KUWAJENGEA NYUMBA ZA KISASA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akizungumza na wakazi 644 waliokuwa wakiishi katika nyumba za Magomeni Kota ambazo zilivunjwa kupisha ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi na Biashara ambao walitelekekezwa kwa muda mrefu na manispaa ya Kinondoni na kuwafanya waishi maisha magumu. Katika hotuba yake Mhe. Rais ameahidi kuwajengea nyumba za kisasa wakazi hao 644 ambapo wataishi bure kwenye nyumba hizo kwa muda wa miaka 5 kabla ya kuandaliwa kwa utaratibu wa kuwamilikisha nyumba hizo. 
******************************


*Wakazi wa Magome Kota kuishi miaka 5 nyumba za kupanga bila kulipa kodi
Na Jonas Kamaleki, Dar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota kukaa kwenye nyumba za Serikali miaka mitano bure na baadaye kuzinunua kwa bei nafuu.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiwahutubia wakazi wa Magomeni na kuagiza ujenzi wa nyumba hizo kuanza ndani ya miezi miwili.
“Nasema wakandarasi ndani ya miezi miwili waanze kujenga nyumba 644 kwa ajili ya wazee ambao wameteseka sana baada ya nyumba zao kuvunjwa, nitatoa fedha Serikalini mwezi huu kwa ajili ya kuanza kwa shughuli hiyo” alisema Dkt. Magufuli. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Ameongeza kusema kuwa ujenzi huu anataka ukamilike ndani ya mwaka mmoja au miezi sita kama ulivyokuwa kwa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema atafurahi kukabidhi hati kwa wakazi wa Magomeni Kota pindi nyumba hizo zitakapokuwa zimekamilika.
“Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uzima ili nyumba hizo zikiwa tayari hati nizikabidhi mwenyewe,”alisema Magufuli.
Rais Magufuli ameonyesha kukerwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu kuwanyima haki wanyonge. Amesema vitendo hivyo vya unyanyasaji viishe mara moja na watanzania wakae kwenye nchi yao kwa amani.
Aidha, Rais Magufuli amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kukusanya madeni yote ya kodi kwa wanaodaiwa na shirika hilo bila kujali chama, serikali au mtu yeyote.
Ameagiza kuwa wanaodaiwa inabidi walipe deni lao ndani ya siku 7 (saba) vinginevyo waondolewe kwenye nyumba hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge hasa kwa kutatua mgogoro wa makazi kwa wakazi wa Magomeni Kota.
“Mheshimiwa Rais ninakushukuru kwa kuwajali wazee hawa wa Magomeni, nami nilitekeleza maagizo yako na kufuatilia mgogoro huu hadi kupata ufumbuzi”, alisema Lukuvi.
Lukuvi amesema kuwa mgogoro wa Magomeni ulivyokuwa mkubwa ulistahili nguvu ya Mhe. Rais Magufuli, lakini kwa migogoro mingine ambayo ni midogo, hiyo ameishughulikia na ataendelea kuishughulikia ili kero za wananchi kuhusu ardhi ziishe kama alivyoagizwa na Rais.
Nyumba zilizokuwa Magomeni Kota zilivunjwa mwaka 2009 na wananchi wakaahidiwa kujengewa nyumba ambazo wangeuziwa kwa bei nafuu. Lakini kwa takribani miaka mitano nyumba hizo hazikujengwa hali ambayo iliwafanya wakazi hao waishi maisha ya kuangaika.
Hivi karibuni Mhe. Rais John Pombe Magufuli alifuta hati zote za umiliki eneo la Magomeni Kota na kuondoa usimamizi wa Nyumba TAMISEMI na kuupeleka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuanza kusimamia ujenzi.Baadhi ya wakazi wa nyumba za Magomeni Kota wakifurahia Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli mara baada ya kuahidi kuzipatia majibu kero zao za muda mrefu. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akizungumza jambo na viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mkoa wa Dar es salaam mara baada ya kuwasili eneo la Magomeni Kota zitakapojengwa nyumba za kisasa za wakazi 644 watakaojengewa nyumba hizo na Serikali. Ujenzi wa nyumba hizo za kisasa unatarajia kuanza mwezi Septemba mwaka huu. KWA PICHA ZAIDI BOFYA READ MORE


Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimweleza jambo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) wakati akikagua eneo zitakapojengwa nyumba za kisasa za wakazi 644 wa eneo la Magomeni Kota ambao watajengewa nyumba na Serikali. Ujenzi wa nyumba hizo za kisasa unatarajia kuanza mwezi Septemba mwaka huu. Wengine Kutoka Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Happi, Mkuu wa Mkoa wa Kinondoni Paul Makonda 9wa pili kutoka kulia na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Aron Kagurumjuli.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia baadhi ya wazee waliokuwa wakazi wa nyumba za Magomeni Kota mara baada ya kuzungumza nao leo jijini Dar es salaam. Mhe. Rais pamoja na mambo mengine ameahidi kuzishughulikia kero zote za wazee hao ikiwemo kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ambazo watakaa bure bila kulipia kwa muda wa miaka 5 na baadaye kufanyika utaratibu wa kuwamilikisha nyumba hizo kwa gharama nafuu.

Baadhi ya wananchi wa jiji la Dar es salaam wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika viwanja vya Magomeni Kota leo.


Msemaji wa Wazee wa Magomeni Kota Mchungaji John Raymond (wa pili kutoka kushoto) akiwa na uso wa furaha akiwa na Wakazi wenzake 644 wa zilizokuwa nyumba za Magomeni Kota ambao wameahidiwa kujengewa nyumba zao na Serikali.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akizungumza na wakazi 644 wa zilizokuwa nyumba za Magomeni Kota ambao ambao nyumba zao zilivunjwa kupisha ujenzi wa mradi wa kisasa wa Makazi na Biashara chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni. Serikali imeahidiwa kuwajengea nyumba wakazi hao kufuatia agizo la Rais.


Baadhi ya akina Baba waliokuwa wakazi wa nyumba za Magomeni Kota wakifurahia Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kufuatia kero na Hoja zao za muda mrefu kupatiwa majibu. 


Baadhi ya Wazee waliokuwa wakazi wa nyumba za Magomeni Kota wakimwombea dua ya Afya njema na Utumishi mwema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kufuatia Hotuba kufuatia hotuba aliyoitoa mara baada ya kuwatembelea eneo la Magomeni Kota kuji kero na Hoja zao za muda mrefu huku akiahidi kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ambazo watakaa bure kwa muda wa miaka 5 kabla ya kufanyika utaratibu wa kuwamilikisha kwa gharama nafuu.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda akizungumza 


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Happi akizungumza na Wakazi 644 wa zilizokuwa nyumba za Magomeni Kota leo jijini Dar es salaam.


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Happi akizungumza na Wakazi 644 wa zilizokuwa nyumba za Magomeni Kota.Picha/Aron Msigwa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.