Habari za Punde

*WIZARA YA ELIMU YAWAASA VIJANA KUTUMIA ELIMU KUJIAJIRI

 Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi  Bw. Nicholaus Bureta akizungumza wakati mkutano wa Vijana wa Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano  wa LAPF leo jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulijadili changamoto za ajira kwa vijana na suala la rushwa.
*****************************************
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imewaasa vijana waliomaliza shule kuacha kujibetweka bali watumie elimu waliyoipata kujitafutia ajira ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Nicholaus Bureta wakati wa ufunguzi wa mkutano wa vijana wa Afrika unaojadili changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Bureta alisema kuwa Serikali  inatoa elimu bora ili kuhakikisha vijana wanapata uwezo na maarifa yatakayowasaidia kujiajiri hata wasipopata nafasi za kuajiriwa katika taasisi na ofisi za umma pamoja na kuitumia elimu hiyo katika kupambana na vitendo vya rushwa.

“Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inatutaka tuwe na watanzania walioelimika na wenye mtazamo chanya ambao utahakikisha jamii yetu inabadilika kufikia uchumi wa kati hivyo vijana msikae kusubiri ajira bali mjifunze jinsi ya kujiajiri kutokana na elimu mliyoipata mashuleni”, alisema Bureta.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN), Stellah Vuzo amewapongeza vijana hao kuamua kukusanyika kuchangia mawazo yao juu ya matatizo yanayowakabili kwani vijana wana nafasi kubwa ya kuhakikisha malengo mbalimbali yanatekelezeka.

Aidha, aliongeza kuwa Umoja wa Mataifa umemteua balozi kijana ambaye anashughulikia ajira za vijana hivyo amewaomba vijana walioshiriki katika mkutano huo kuyafikisha mawazo hayo kwa balozi huyo ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

Naye Mkuu wa Utafiti kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB), Daniel Pundu alisema kuwa tatizo la rushwa haliwezi kuisha endapo vijana hawatashirikishwa hivyo amewasisitiza vijana kushirikiana na Serikali kuchukua hatua za kupambana na rushwa ili kuhakikisha rushwa inaondoka.

“Tunajua kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa na ndio sababu tunawasisitiza kupambana na rushwa, kwa kulitambua hilo Serikali imeanzisha vilabu vya wapinga rushwa katika shule za sekondari na vyuo vikuu vikiwa na lengo la kuhakikisha vijana wanahusika kwenye mapambano hayo”, alisema Pundu.
Washiriki wa Mkutano wa Vijana wa Afrika wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mkutano wa Vijana wa Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano  wa LAPF leo jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulijadili changamoto za ajira kwa vijana na suala la rushwa
Kaimu Kamishna wa Elimu Bw. Nicholaus Bureta akinyanyua juu nembo ya African Youth Leadership Transformation Summit (AYLTS) kuashiria uzinduzi wa nembo ya taasisi hiyo wakati wa hafla iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Kamishna wa Elimu Bw. Nicholaus Bureta akiwa kwenye picha ya pamoja na waandaaji wa Mkutano wa Vijana wa Afrika juu ya changamoto za ukosefu wa ajira na rushwa pamoja na suluhu za changamoto katika ukumbi wa Mikutano wa LAPF ulioko Millenium Tower jijini Dar es Salaam. Picha Na: Lilian Lundo – MAELEZO

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.