Habari za Punde

*YANGA WAENDELEZA DOZI YA 3=0 TENA DHIDI YA MAJIMAJI UWANJA WA UHURU DAR

BAADA ya kikao cha dharula na mwenyekiti wake Yusuf Manji majuzi, leo timu ya Yanga imefanya kile walichokitarajia mashabiki wake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Majimaji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Yanga leo wameshuka dimbani kuchezamchezo wao wa tatu wa Ligi Kuu huku mchezo wa kwanza wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon,na mchezo wa pili wakiambulia sare ya 0-0 dhidi ya Ndanda Fc uliopigwa wiki iliyopita mjini Mtwara.

Bao la kwanza leo lilifungwa na Deus Kaseke katika dakika ya 20, aliyemalizia kwa kuuwahi mpira wa penalti iliyopigwa na Simon Msuva, ambapo mwamuzi wa mechi hiyo Emmanuel Mwandebwa wa kutoka Arusha alitoa penalti kwa Yanga baada ya mchezaji wa Majimaji kushika mpira eneo la hatari na ndipo Msuva alipopiga penalti mara ya kwanza, lakini mwamuzi alimtaka kurudia tena akidai alikosea, akaipiga mara ya pili ikaamuliwa kurudia tena, akapiga mara ya tatu mpira ukagonga mwamba na ndipo Kaseke alipouwahi na kuujaza wavuni.

Ilikuwa ni dakika ya 74, mwamuzi alikataa bao la Amisi Tambwe na katika dakika ya 81, Mrundi huyo alipowainua tena mashabiki wa Yanga kwa kufunga bao la pili  kwa kichwa, na dakika tano baadaye, Tambwe aliongeza bao la tatu akiitendea haki pasi ya Juma Mahadhi na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Na Matokeo mengine kutoka Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Azam wameendeleza ubabe kwa timu za jiji hilo kwa kuibuka ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City na kutimiza hazma yao ya kuondoka na pointi zote 6 katika uwanja huo kama walivyoahidi.

Na huko mjini Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ndanda Fc nao wameendelea na kuambulia sare ya 0-0 na Kagera Sugar. 

Mjini Shinyanga, Mwadui Fc nao wametoka sare ya 2-2 na Stand United.

Katika uwanja wa Mabatini Mlandizi, Ruvu Shooting iliitambia JKT Ruvu kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ligi hiyo inaendelea tena kesho kwenye uwanja wa Uhuru ambapo Simba itawakaribisha Mtibwa Sugar.
Timu hizo zinakutana zikiwa na makocha wapya Joseph Omog wa Simba na Salum Mayanga wa Mtibwa na wote wakionesha kuwa wanalitaka taji kulingana na ubora wa vikosi vyao.

Mtibwa Sugar inapokutana na Simba au Yanga ni wazi kuwa hucheza kwa kukamia, lakini mwisho wa siku mmojawapo huibuka na ushindi.

Msimu uliopita timu hizi zilikutana raundi ya kwanza Januari 16, mwaka huu Simba ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, pia ilipokutana katika raundi ya pili Mei 15, mwaka huu bado Simba ilishinda bao 1-0.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.