Habari za Punde

*YANGA WAMKATIA RUAA FRANK KHAMIS IGOBELA WA STAND UNITED KUCHEZA MECHI DHIDI YAO

KLABU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, imewasilisha barua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga klabu ya Stand United kumtumia mchezaji Frank Khamis Igobela katika mchezo wa Jumapili.

Yanga ilifungwa 1-0 na Stand United Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na baada ya mchezo ikawasilisha rufaa.

Yanga inadai Stand United imemtumia Igobela kimakosa kwa kuwa bado ni mchezaji halali wa Polisi ya Zanzibar.

Chanzo cha habari kutoka Yanga SC kimesema kwamba, klabu imepata taarifa za kutosha kutoka Polisi ya Zanzibar juu ya mchezaji huyo.

Na Yanga wanadai kwamba wana ushahidi hadi wa barua ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kikiizuia TFF kumuidhinisha mchezaji huyo kucheza Ligi Kuu hadi amalizane na Polisi.

Na Yanga wanadai wanaamini Igobela alicheza mechi ya Jumapili akiwa hana leseni, lakini wamejaribu kufuatilia TFF tangu jana hawajapata majibu.

Yanga iliondoka Shinyanga Alfajiri ya jana kwenda Mwanza kuunganisha ndege ya kuwapeleka Dar es Salaam, baadaye Pemba kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo ujao, dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Na wakati ikiendelea na maandalizi ya mchezo huo wa Jumamosi, Yanga inayofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm inapigania ushindi wa mezani baada ya kipigo cha Stand kilichotokana na bao pekee la Athanas Pastory.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.