Habari za Punde

CHUO CHA TAKWIMU MASHARIKI MWA AFRIKA CHAZINDUA MAFUNZO MAALUMU YA UKUSANYAJI TAKWIMU RASMI.

 Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Prof. Innocent Ngalinda akizungumza na washiriki wa mafunzo na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mafunzo maalumu ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi uliofanyika leo katika chuo hicho kilichopo Changanyikeni jijini Dar es salaam.
 Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Dkt. Frank Mkumbo akizungumza na washiriki wa mafunzo na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mafunzo maalumu ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi uliofanyika leo katika chuo hicho kilichopo Changanyikeni jijini Dar es salaam.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo maalumu ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Prof. Innocent Ngalinda wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika leo katika chuo hicho kilichopo Changanyikeni jijini Dar es salaam.
************************************
Na: Albert Fen, Dar es Salaam
Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Prof. Innocent Ngalinda amezindua mafunzo maalumu ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi ambayo yalianza tarehe 17 Oktoba mwaka huu chuoni Changanyikeni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Prof. Ngalinda amesema   mafunzo hayo yameandaliwa kwa nia ya kumpatia mshiriki ujuzi katika ukusanyaji takwimu kwa ajili ya kuzichakata na kuwa takwimu rasmi. 

“Washiriki hawa watafundishwa mbinu shirikishi, utatuzi wa matatizo mbalimbali wakati wa ukusanyaji takwimu, sensa na viwango vya tafiti mbalimbali, utunzaji wa Vifaa vya ukusanyaji takwimu kama vile simu za mkononi  na kumpyuta mpakato pamoja na kubadilisha madodoso ya kawaida na kuwa ya kisasa”, amesema Prof. Ngalinda.

Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa chuoni hapo Dkt. Frank Mkumbo amesema lengo ni kuwawezesha wakusanyaji takwimu kukusanya takwimu halisi na zenye ubora kwa ajili ya kupanga mipango mbalimbali ya Maendeleo.

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa wakusanyaji takwimu rasmi wanakuwa na weledi wa kutosha katika kukusanya takwimu bora na zenye tija kwa taifa” amefafanua Dkt. Mkumbo.

Jumla ya washiriki 110 wamejiunga na mafunzo hayo maalumu ya muda wa miezi miwili kwa awamu ya kwanza ambayo yatamalizika mwezi Disemba, 2016 na watakaomaliza na kufaulu watapatiwa cheti cha Ukusanyaji Takwimu. Awamu ya pili ya mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza Novemba mwaka huu na kumalizika Januari, 2017.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.