Habari za Punde

KOCHA MSAIDIZI WA MBEYA CITY KIJUSO ASEMA WAMEJIANDAA KUFUTA MAKOSA MLANDIZI

KOCHA msaidizi wa kikosi cha Mbeya City fc, Mohamed Kijuso amesema kuwa makosa kadhaa aliyojitokeza na kuigharimu timu yake katika mchezo uliopita dhidi ya Simba Sc yamefanyiwa kazi na hayatajitokeza katika jumapili hii wakati itakaposhuka dimbani kucheza dhidi ya wenyeji Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi, mkoani Pwani.

Akizungumza asubuhi ya leo kabla ya kikosi hicho kuanza safari kulekea Mlandizi, kocha Kijuso alisema kuwa, baada ya kupoteza mchezo na Simba, bechi la ufundi lilitumia saa kadhaa kunagalia mkanda wa video (CD) wa mchezo huo na kubaini makosa kadhaa yaliyosababisha kufungwa mabao hayo 2 na Simba katika kipindi cha kwanza.

“Kama uliona mchezo unaweza kukumbuka kuwa tulicheza vizuri sana kipindi cha pili lakini hatukuwa na mwanzo mzuri katika dakika 45 za kwanza, baada ya mchezo tulilazimika kupitia mkanda na tumebaini makosa kadhaa, haraka tumeyafanyia kazi na imani yangu makosa yote tutayafuta jumapili na kupata ushindi dhidi ya wapinzani wetu”, alisema.

Akiendelea zaidi Kocha huyo msaidizi aliweka wazi kuwa kuwa na majeraha kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kulilazimu benchi la ufundi kubadili mfumo jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine pia liliongeza nafasi kwa Simba kupata mabao hayo ya haraka haraka kipindi cha kwanza.

“Tulikuwa na wachezaji kadhaa majeruhi ambao walikosa mchezo, tulilazimika kubadili mfumo lakini baada ya kipindi cha kwanza tukabaini kuna makosa ndiyo sababu tukarekebisha na timu ikafanikiwa kucheza mchezo mzuri kipindi cha pili ingawa hatukufanikiwa kupata bao,yote tumeyaona na tayari tushayafanyia kazi imani yangu kuwa tutapata matokeo mazuri jumapili” alimaliza.

Katika hatua nyingine Ofisa habari, Dismas Ten ameudokeza mtandao huu kuwa kikosi chake kimeanza safari asubuhi ya leo kuelekea Dar Salaam tayari kwa mchezo wa jumapili dhidi ya Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

“Tumeondoka asubuhi hii kuelekea Mlandizi, tutapita moja kwa moja mpaka Dar ambapo tutaweka kambi yetu kwa ajili ya matayarisho ya mwisho ya mchezo wa jumapili, kijografia Dar na Mlandizi si mbali pia ni maeneo ambayo hali ya hewa ina fanana kwa maana hiyo tumeona ni sehemu nzuri ya kupata utulivu kwa ajili kujiwinda na mchezo huo” alisema.

“City imeondoka Mbeya na kikosi cha wachezaji 20 na viongozi 10 watakaoongoza kampeni za kusaka ushindi kwenye mchezo huo” aliongeza.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.