Habari za Punde

MICHEZO YA SHIMIWI YA MWAKA 2016 YAAHIRISHWA

SHIRIKISHO LA MICHEZO YA WIZARA NA IDARA ZA SERIKALI

TAARIFA KWA UMMA

KUAHIRISHA MICHEZO YA SHIMIWI KWA MWAKA 2016
Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) katika Kalenda ya mwaka 2016 ilipanga michezo ya SHIMIWI ifanyike mkoani Dodoma kuanzia tarehe 14-27 Novemba, 2016.

Kama mnavyofahamu hivi karibuni Taifa limekumbwa na janga la tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.  Janga ambalo limesababisha vifo, limeacha familia nyingi kukosa makazi.  Tetemeko hili limeleta madhara makubwa. Taasisi, Mashirika, nchi mbalimbali na watu binafsi wameguswa kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko ili kukabiliana na madhara yaliyotokea. 
Katika kutimiza dhamira ya kuleta maendeleo katika Taifa Serikali  ya awamu ya tano imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuleta ufanisi.  Zikiwemo kuahirisha Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru ili fedha ambazo zingetumika zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na vile vile imeelekeza kuhakikisha azma ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma inatimizwa.

Majukumu yote niliyoyataja yanategemea Mapato ya Serikali.  Vile vile gharama za kuendesha Michezo ya SHIMIWI kwa kiasi kikubwa zinatokana na Bajeti ya Serikali.  Tunapenda kuwaarifu Wananchi, Wanamichezo wote na Watumishi wa Umma wote kuwa kwa kuzingatia majukumu yote ambayo Taifa inayatekeleza kwa sasa SHIMIWI imeamua kuunga mkono kwa kuahirisha michezo ya SHIMIWI  kwa mwaka huu 2016 ili kushirikiana kuelekeza nguvu pamoja na makundi mengine ya kijamii wakiwemo Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu hayo.  Tunawashauri watumishi wote waendelee kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga afya zao kupitia ushiriki wa pamoja kwenye Bonanza la Wafanyakazi wa Umma katika maeneo yao katika siku za mwisho wa wiki.

Vile vile naomba nitumie fursa hii kusisitiza vilabu wanachama vihakikishe vinalipa ada ya mwaka kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa mwaka utakaofanyika Januari, 2017.  Hadi sasa ni timu chache zimekwishalipa.  Kumbukeni kwamba kwa mujibu wa katiba ya SHIMIWI wanachama watakaoshiriki kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka ni wale waliolipa ada ya mwaka.  

 Daniel Mwalusamba
MWENYEKITI - SHIMIWI - TAIFA
11 Oktoba, 2016
KWA PAMOJA MAKUNDI YOTE YA KIJAMII
TUSHIRIKIANE KULIJENGA TAIFA LETU TANZANIA

MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.