Habari za Punde

MZEE AKILIMALI 'NJE NDANI' MKUTANO MKUU, MANJI AWATAKA WANACHAMA KULIPA ADA NA KUJITOKEZA KWA WINGI JUMAPILI

Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
MZEE maarufu wa Yanga, almaaruf Mzee Akilimali, hati hati kuhudhuria mkutano mkuu wa dharula wa Yanga unaotarajia kufanyika siku ya jumapili Okt. 23, kutokana na kutotimiza vigezo na masharti ya uanachama.

Imebainika kuwa Mzee Akilimali hadi sasa hajalipa ada ya Uanachama ya miezi sita, ambapo ametakiwa kulipia ada hiyo kabla ya siku hiyo ya mkutano mkuu ili aweze kukidhi vigezo vya kuhudhuria mkutano huo.

Hayo yamebainika leo wakati Mwenyekiti wa Yanga Yusuf  Manji, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kumtaka mzee Akilimali kulipia ada yake hiyo ya miezi sita.

Manji amewataka wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mkutano mkuu wa dharula siku hiyo ya jumapili Oktoba 23, kwenye  Uwanja wa Kaunda Makao makuu ya Jangwani.

Manji alisema kuwa wanachama wote wajitokeze siku hiyo ili kufanikisha mkutano huo ikiwa ni njia mojawapo ya kuijenga Yanga Imara kwa wanachama kuchangia katika suala la maendeleo ikiwemo mabadiliko yanayotarajiwa kujitokeza ya kwenda kwenye mfumo mpya wa uendeshaji wa kutoka mikononi mwa wanachama na kwenda kampuni ya Yanga Yetu.

Mkutano huo wa dharula wenye ajenda 13, ikiwemo ya mabadiliko ya uendeshaji  pamoja na hatma ya Mwenyekiti wa klabu hiyo kuendelea na nafasi yake au kujiuzulu umekuwa ukizungumziwa sana katika vyombo vya habari na baadhi ya wanachama kupinga mabadiliko hayo na hata kutaka Mwenyekiti huyo ajiuzulu wadhifa wake.

Aidha Manji alisema kuwa, kujitokeza kwa wingi kwa wanachama kutasaidia kujadiliana kwa hoja na kupata mapendekezo yao na kulingana na katiba ya Yanga mwanachama ambaye hajalipia ada yake kwa kipindi cha miezi sita anakuwa amejifuta uanachama na atatakiwa kuomba upya uanachama katika tawi lake.

Akiongelea suala la Uwanja wa mazoezi, Manji amesema kuwa katika makubaliano ya mkataba wao ujenzi wa Uwanja huo utaanza kujengwa ndani ya siku 90 katika eneo la Gezaulole lililopo Kigamboni.

Aidha Manji amesema kuhusu suala la kusainiwa kwa mkataba na bodi ya wadhamini dhidi ya kampuni ya Yanga Yetu kila kitu kitajadiliwa kwenye mkutano huo

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.