Habari za Punde

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YAPANIA KUBORESHA ZAIDI UPATIKANAJI WA TAKWIMU RASMI NCHINI.

Na: Mwandishi wetu 
Wadadisi au wakusanyaji taarifa za kitakwimu rasmi katika tafiti mbalimbali zinazoratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wametakiwa kuwa wamehitimu Mafunzo ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi angalau kwa ngazi ya cheti.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa imesema matakwa hayo ni kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na. 9 ya mwaka 2015 inayoipa mamlaka ofisi hiyo ya kuratibu na kusimamia ukusanyaji wa Takwimu rasmi nchini.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa utumiaji wa wadadisi ambao wamepitia mafunzo ya ukusanyaji takwimu angalau kwa ngazi ya cheti kutasaidia kuboresha zaidi upatikanaji wa takwimu rasmi nchini. 

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa Mafunzo ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi yanatolewa na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika "Eastern Africa Statistical Training Centre (EASTC) kilichopo Changanyikeni jijini Dar es Salaam.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kukusanya, kuchambua na kusambaza Takwimu Rasmi Nchini kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.