Habari za Punde

WAZIRI MAKAMBA ASISITIZA MATUMIZI YA MAJIKO BANIFU KATIKA UKAUSHAJI WA TUMBAKU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akifafanua jambo kuhusu wananchi waliovamia msitu wa hifadhi ya Kijiji. Kushoto ni Bi. Veronica Nyasa mkazi wa eneo hilo ambae amesema yuko tayari kuondoka endapo atapatiwa sehemu mbadala.
Uongozi wa Wilaya ya Kaliua wakimwonyesha Waziri Makamba magogo ya miti ya asili yanayotumiwa na wanachi katika kukaushia tumbaku kwa kutumia majiko ya kienyeji
Pichani ni moja ya majiko ya kienyeji yanayotumia kuni/miti mingi katika kukaushia tumbaku. Waziri Makamba amewaagiza wakazi wa Kitongoji cha Mtakuja Magharibi kutumia majiko banifu ili kunusuru ukataji miti kwa wingi husnan ile ya asili
******************************************
Na Lulu Mussa-Tabora
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira hii leo ameendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoani Kigoma.

Akiwa Mkoani Tabora Waziri Makamba ametembelea Wilaya ya Kaliua na kukutana na changamoto kubwa ya Uharibifu wa Mazingira na Uvamizi wa Misitu unaofanywa na wananchi. Katika Kijiji cha Ufugala Wilaya ya Kaliua Waziri Makamba amefanya Mkutano wa hadhara kijijini hapo na kubaini kuwa Kitongoji hicho hakikufuata taratibu za kisheria katika kuanzishwa kwake na kimeanzishwa ndani ya Hifadhi.

Akitoa maelezo ya Awali Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abel Yeji Busalama amemueleza Waziri kuwa Kitongoji hicho kiko ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Kijiji ambapo jumla ya Vijiji 11 viamua kutenga eneo hilo kwa ajili ya Hifadhi.

Bw. Busalama amesema kuwa wakazi hao wamekwisha amriwa kuondoka katika hifadhi hiyo na utekelezaji wake unaendelea.

Akijibu hoja zilizowasilishwa na wakazi wa eneo hilo Waziri Makamba amesema kuwa wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kuwa Sheria, tararibu na kanuni zinafuatwa bila kukiukwa. Waziri Makamba pia amesisitiza kuwa maamuzi ya matumizi bora ya ardhi yapo mikononi mwao. “Ndugu zangu ni nyinyi wenyewe mliamua kutenga eneo hili maalumu kwa hifadhi ya msitu wa kijiji na kufuata taratibu zote za kisheri katika kuusajili, maamuzi yenu ya awali yatabaki palepale mpaka mtakapofuata taratibu nyinginezo.” Makamba alisisitiza.

Aidha, Waziri Makamba ameahidi kuwasilisha suala hilo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kupata ufumbuzi wa kudumu. “Nitaongea na Mawaziri wenzangu na kuleta timu ya wataalumu kupitia upya mipaka ya kijiji na kuifanyia kazi” Makamba alisisitiza.

Kuhusu hifadhi ya Mazingira Waziri Makamba amewataka wakazi wa Ufulaga kuacha tabia ya kukata miti ya asili na kusisitiza kuwa uharibifu wa mazingira unabadilisha tabia za watu. “Wana Ufulaga, binadamu wakiharibu mazingira kwa kiasi kikubwa wanaanza wizi na udokozi na wanyama wataanza kuwinda watu kwa kukosa malisho” alisema Waziri Makamba.

Waziri Makamba pia amefanya ziara katika Wilaya ya Urambo na kubaini changamoto kubwa ya uvamizi wa misitu na ukataji wa miti ya asili kwa ajili ya kuni za kukaushia tumbaku.

Waziri ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutumia Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu namba 196 (1) (a na b) kupiga marufuku ya matumizi ya majiko banifu ya kienyeji pia ukataji mkubwa wa miti ya asili kwa ajili ya biashara ya tumbaku. Katazo hilo litawahusu Wakulima na Vyama vya Msingi vyote vinavyojishughulisha na biashara ya tumbaku.

Waziri Makamba anaendelea na ziara yake kwa kutembelea Wilaya za Nzega na Igunga.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.