Habari za Punde

BUNGE LAPATA MSIBA WA GHAFLA

Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar Mhe. Hafidh Ali Tahir katika enzi za uhai wake.
******************************************
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata msiba wa gafla wa Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar Mhe. Hafidh Ali Tahir aliyefariki leo majira ya saa 8 usiku kwa ugonjwa wa moyo katika Hospitali ya General iliyopo mkoani Dodoma.
Taarifa hiyo imetangazwa leo Bungeni mjini Dodoma na Spika wa Bunge hilo, Mhe. Job Ndugai na kusitisha shughuli za Bunge kwa ajili ya kupisha shughuli za kuuaga mwili wa Mbunge huyo zilizofanyika katika viwanja vya Bunge vilivyopo mjini humo kuanzia saa 3:30 asubuhi na kupelekwa uwanja wa ndege wa Dodoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi yatakayofanyika leo Novemba 11 mwaka huu.

Mhe, Ndugai amesema kuwa marehemu Mhe. Hafidh Ali aliugua kwa muda mfupi ambapo baada ya kujisikia vibaya aliamua mwenyewe kuelekea Hospitali ndipo huko mauti yalipomkuta wakati akiendelea na matibabu Hospitalini hapo.  
“Ndugu waheshimiwa wabunge kwa masikitiko makubwa naomba kuwatangazia msiba tulioupata wa Mbunge mwenzetu Mhe. Hafidh Ali aliyefariki leo usiku katika Hospitali ya mkoa wa Dodoma, kwa kweli tumeondokewa na Mbunge mchapakazi, mwanamichezo, mcheshi na aliyewajali wapiga kura wake kwa kiasi kikubwa”, alisema Mhe. Ndugai.

Akitoa salamu za rambirambi kwa upande wa Serikali, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa pole kwa wafiwa wote kwa kumpoteza mtu mahiri aliyeshirikiana na wenzake katika shughuli mbalimbali za kitaifa pamoja na kijamii.
“Ni jambo la huzuni sana kwa Bunge letu na Serikali kwa ujumla kwa sababu Mbunge mwenzetu alikua mchapakazi na alijitahidi kushiriki katika kamati nyingi za Bunge hasa Kamati ya PAC, hii inaonyesha dhahiri kuwa marehemu alikuwa ni mtu anaejali wenzake na wenzake wanathamini mchango wake katika shughuli hizo”, alisema Waziri Mkuu.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Kiongozi wa kambi hiyo Mhe. Freeman Mbowe amesema kuwa Bunge limempoteza Mbunge, Mwanamichezo pamoja na kiongozi hodari kwa kuwa katika kipindi cha uhai wake alijitahidi kutoa mawazo chanya katika maamuzi mbalimbali ya maendeleo pia aliishi vizuri bila kumbagua mtu kutokana na itikadi za vyama.
“Mhe. Hafidh Ali amemaliza safari yake hapa duniani hivyo kifo chake ni kama somo kwa sisi tuliobaki, katika kipindi cha uhai wetu tutambue kuwa tofauti zetu ni za muda mfupi hivyo natoa rai kwa wabunge wote kuungana na kuwa kitu kimoja ili kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya nchi yetu bila kujali itikadi ya vyama vyetu”, alisema Mhe. Mbowe.
Akiwakilisha Timu ya mpira wa miguu ya Bunge (Bunge Sports Club), Mwenyekiti wa timu hiyo, Mhe. William Ngeleja amesema kuwa marehemu alikuwa mwanamichezo mahiri wa mpira wa miguu na muda mwingi wa maisha yake aliutumia katika michezo.

“katika enzi za uhai wake, marehemu aliwahi kuwa Mchezaji, Kocha na Mwamuzi wa mpira kwa kiwango cha kimataifa wa timu yetu ya Bunge pia amewahi kupata fursa za kuchezesha fainali za kombe za mataifa ya Afrika mara 9 pamoja na fainali za kombe la Dunia kwa watoto chini wa miaka 17 hivyo wanamichezo tumepata pigo kubwa sana”,alisema Mhe. Ngeleja.

Marehemu Hafidh Ali Tahir alizaliwa Octoba 30 mwaka 1953 mjini Unguja, alimaliza Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Bondeni, Unguja mwaka 1966 baadae mwaka 1985 alisoma masomo ya Habari na Utangazaji. Mnamo mwaka 1995 alianza shughuli za siasa ambapo mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar aliyeliongoza jimbo hilo hadi mauti yalipomfika.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.