Habari za Punde

CHUO CHA VETA MIKUMI KUANZISHA KOZI YA UTALII WA KIUTAMADUNI


Mwalimu wa Ufundi Mitambo wa Chuo cha VETA Mikumi, Peris Shao, akiwaelekeza jambo waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya chuo hicho katika utoaji wa mafunzo ya ufundi Stadi.

Wanafunzi wakiwa katika karakana ya ufundi Mitambo kwenye mafunzo ya vitendo Chuo cha Mikumi

Mwalimu wa Chuo cha VETA Mikumi, James Maungu, akitoa maelezo kwa waandishi wa habari walipotembelea Karakana ya ufundi huo.
Mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa Chuo cha VETA Mikumi wakiwa katika mafunnzo ya vitendo karakana ya ufundi wa Magari.
*******************************************************
MAMLAKA ya Elimu na mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) kupitia chuo cha VETA Mikumi inatarajia kuanzisha kozi ya utalii wa kitamaduni ili kuwafundisha watanzania tamaduni ,mila na desturi ili kuulinda utamaduni wa Mtanzania, ambao unaonekana kupotea kadri teknolojia inavyozidi kukua siku hadi siku.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotemebelea chuo hicho Cha VETA Mikumi, mjini Morogoro, Mkuu wa chuo hicho Christopher Ayo, alisema kuwa uamuzi huo umetokana na sekta ya utalii kuendelea kukua mwaka hadi mwaka huku jamii ikionekana kusahahu uhasilia wa tamaduni mbalimbali za kitanzania .

Aidha alisema kuwa utamaduni ukitumika ipasavyo unaweza kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii pamoja na uchumi nchini kutokana na ukweli kwamba nchi nyingi duniani zimeweza kulinda tamaduni zao na kuweza kukuza uchumi wao.

Amesema chuo chake kwa kushirikiana na Chuo cha NOVA Scotia Communinity College cha nchini Canada kinaandaa kozi hiyo itakayowezesha watanzania kujifunza kwa undani kuhusu utamaduni wao kama vile ngoma, vyakula vya asili ,sanaaa na historia ya makabila mbalimbali.

Ayo amesema maandalizi ya kuanza kwa kozi hiyo yapo kwenye hatua za mwisho na kwamba kuanzia Januari, 2017 masomo yataanza kutolewa.

Aidha mkuu huyo amesema walimu watano watakaofundisha masomo hayo wameshaandaliwa na kupatiwa mafunzo nchini Canada jinsi ya kutumia technologia katika kufundisha na kuandaa mitaala.

Ayo amesema VETA Mikumi itaendelea kutoa mafunzo kwa jamii inayowazunguka katika kuwaandaa vijana katika soko la ajira kwa kujiajiri au kuajiriwa na kuweza kuendesha maisha yao na kuchangia pato la taifa.

Ametoa rai kwa vijana wa mikumi na maeneo ya mengine ya Mkoa wa Morogoro kuchangamkia fursa za mafunzo zilizopo chuoni hapo ili kuweza kuwa sehemu ya wataalam watakaohudumia viwanda vitakavyojengwa kutokana na serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuweka msisitizo wa kuhakikisha nchi inakuwa ya viwanda.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.