Habari za Punde

IDADI YA WANAFUNZI WASIOMUDU KKK YAPUNGUA MKOANI SIMIYU

Na. Lilian Lundo – MAELEZO - Simuyu
Idadi ya wanafunzi wasiomudu Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) Mkoani Simiyu imepungua kutoka wanafunzi 18,216 Machi, 2016 kufikia wanafunzi 1,614 Septemba, 2016.

Afisa Elimu wa Mkoa huo, Julius Nestory ameyasema hayo leo, Mjini  Bariadi alipokuwa akifungua mafunzo kwa Maafisa wa Serikali za Mitaa wa Mkoa huo inayohusu  Mawasiliano na Kushirikishana Jitihada zenye mafanikio kwenye Elimu.

“Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) umeiletea mafanikio makubwa Mkoa wa Simuyu ambapo mpaka Machi, 2016 Mkoa ulikuwa na jumla ya wanafunzi 18,216 ambao walikuwa hawamudu KKK, idadi hiyo imepungu na mpaka kufikia Septemba, 2016 jumla ya wanafunzi 16,602 walimudu KKK,” alifafanuna Afisa Elimu huyo.

Aliendelea kwa kusema kuwa, mafanikio hayo yamechochewa na kampeni ya Mkoa ya kumaliza tatizo la kutokujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la Tatu hadi la Sita ambapo walianza kwa kuwabaini wanafunzi hao kwa majina na kuwaanzisha madarasa maalum ya KKK.

Hivyo basi walimu waliojengewa uwezo wa mbinu za kufundisha KKK kupitia mpango wa EQUIP-T walitumika kuwafundisha wanafunzi hao ambao waliwekwa katika madarasa ya wasiojua  KKK  na kutolewa katika madarasa hayo mara baada ya kuzimudu KKK.

Vile vile Afisa Elimu huyo alisema kuwa, wanafunzi hao wamekuwa wakifundishwa  muda wa ziada wa kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 9:30 ambapo wazazi waliombwa kuwasaidia chakula wanafunzi hao kwa kuwa walitakiwa kuendelea kuwepo shuleni hata baada ya muda wa masomo ya kawaida kumalizika.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Bariadi Mji, Peter Ernest amesema kuwa Wilaya hiyo ilikuwa na jumla ya wanafunzi 1,846 wa darasa la Tatu hadi Sita wasiomudu KKK mpaka kufikia Aprili, 2016.

Wilaya ilianzisha madarasa rekebishi ambapo wanafunzi hao walifundishwa namna ya kumudu KKK na kufikia Octoba, 2016 wanafunzi wote 1,846 waliweza kumudu KKK.

Mkoa wa Simuyu ni moja ya mikoa saba iliyoko katika Mpango EQUIP-T, mikoa mingine iliyoko katika mpango huo ni  Dodoma, Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mara na  Lindi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.