Habari za Punde

KIUNGO SEMTAWA KUIKOSA YANGA, KUKAA NJE WIKI MBILI

KIUNGO mahili wa Mbeya City Fc , Ayoub Semtawa atalazimika kusubiri kwa majuma mawili zaidi kuweza kurejea uwanjani, kufutia majeraha ya kuchanika nyama za paja mguu wake wa kulia kwenye mchezo dhidi ya African Lyon uliochezwa jijini Dar,wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa daktari wa kikosi, Dr Selaphini Mushi, Semtawa alichanika vibaya nyama za paja baada ya kugongwa na mlinzi wa Lyon wakati alipokuwa akijaribu kukontroo mpira wa juu na kulazimika kutolewa nje kwa msaada baada kushindwa kabisa kutembea kufuatia tukio hilo lililotokea kwenye dakika ya 60 ya mchezo huo.

“Baada ya kutolewa ilitulazimu kumpa magongo ili aweze kutembea kwa sababu alikuwa hawezi, juma moja limepita sasa ameacha kutumia magongo na anaweza kutembea mwenyewe, taratibu za matibabu zinaendelea lakini atalazimika kusubiri wiki mbili zaidi ili kuweza kurejea kwenye hali yake ya kawaida na hatimaye kuingia tena uwanjani, hatuna shaka sana na hali yake kwa sasa na imani yangu kubwa baada ya muda huo atakuwa tayari kwa kuitumikia timu” alisema.

Katika hatua nyingine Dr Mushi alithibitisha kupona na kuanza mazoezi kwa golikipa Owen Chaima ambaye alitolewa nje kwenye mchezo uliopita dhidi ya Majimaji kufutia maumivu makali ya mgongo aliyopata wakati akiwa kwenye mchezo.

“Chaima alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Fikirini Bakari, alipata maumivu makali wakati akiwa kwenye mchezo, jambo jema ni kuwa baada ya matibabu sasa yuko fiti kabisa na amefanya mazoezi siku ya jana na leo atafanya pia kwa ajili ya kujiweka sawa tayari kwa mchezo dhidi ya Yanga hapo kesho kama ilivyo kwa mshambuliaji Geofrey Mlawa ambaye naye aliumia lakini sasa yuko kwenye hali nzuri kabisa” alimaliza.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.