Habari za Punde

KOCHA LWANDAMINA ARITHI RASMI MIKOBA YA PLUIJM ALIYEKUBARI KUWA MKURUGENZI BENCHI LA UFUNDI YANGA,

HATIMAYE uongozi wa klabu ya Yanga umeweka wazi mrithi wa Kocha Pluijm George Lwandamina kutoka Zambia ambaye ametua nchini kurithi mikoba ya mholanzi Hans Van De Pluijm aliyekubari kuwa mkurugenzi wa benchi la Ufundi wa Klabu hiyo.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha Redio cha EFM, Makamu mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga, ameweka wazi kuwa kuwa ni kweli wameingia mkataba na George Lwandamina aliyekuwa akiifundisha Zesco United ya nchini Zambia na rasmi ataanza kuinoa timu hiyo mzunguko wa pili wa ligi kuu.

Sanga mbali na kuweka wazi suala hilo ambalo lilikuwa ni gumzo kwa vyombo vya habari nchini, pia ametoa maelezo ya kina kwa mustakabali wa aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Hans Van Pluijm na kusema kuwa bado ataendelea kubaki katika Klabu hiyo na kuwa Mkurugenzi wa benchi la ufundi.

''Kama mnavyojua Pluijm ni mwalimu mzoefu na anaijua vyema Yanga hivyo ushauri wake na uzoefu utakuwa chachu ya mafanikio katika benchi letu la ufundi na klabu kiujumla'' alisema Sanga.

Hans Van Pluijm ameridhia nafasi hiyo baada ya uongozi wa klabu hiyo kukaa nae chini na kumwomba kuendelea kubaki klabuni hapo katika nafasi hiyo adhimu kwa maendeleo ya klabu kimbinu na kiufundi na mabadiliko hayo hayana maana kwamba kiwango cha kocha huyo wa awali kilikuwa kibaya bali uongozi katika hatua ya kuiboresha klabu yake umeamua kuleta changamoto mpya ili kujiweka bora zaidi katika michuano mbalimbali inayoikabili timu hiyo.

Wakati huo huo makamu mwenyekiti amezungumzia hatima ya kocha msaidizi wa klabu hiyo ndugu Juma Mwambusi bado wanamtambua kama kocha msaidizi wa klabu hiyo mpaka hapo itakapotangazwa tofauti. 

"mara nyingi kocha mkuu ndio anaamua au kupendekeza msaidizi wake na sio klabu hivyo bado Mwambusi ni kocha wetu mpaka hapo itakapotangazwa tofauti . Klabu kwa sasa imejikita kwa hao wawili wakubwa wa juu", amesema Sanga.
Kocha Hans Van De Pluijm pamoja na msaidizi wake Juma Mwambusi wameifikisha timu hiyo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ikiwa nyuma ya wahasimu wao wakubwa Simba SC kwa tofauti ya alama 2 ambapo Simba, wanaongoza ligi wakiwa na alama 35 na Yanga 33, kwa sasa uongozi wa Yanga unaandaa siku maalumu ya kuwatambulisha George Lwandamina kama kocha mkuu na Hans Van Pluijm kama mkurugenzi wa ufundi wa klabu kwa wanachama , wapenzi na wadau wa soka nchini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.