Habari za Punde

MNYAMA SIMBA AFIA KWA WAJELAJELA MBEYA APIGWA 2-1, AZAM FC YACHANUA 4-1 SHINYANGA

Tanzania Prisons 2 - Simba SC 1
Mwadui Fc 1 - Azam Fc 4

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Bara leo ulikuwa na mechi mbili ambapo Simba Mnyama alikuwa ugenini kule Mkoani Mbeya akimenyana na Tanzania Prisons, katika mchezo wake wa kumalizia mzunguko wakwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. 

Katika mchezo huo Simba amekubali kichapo cha mabao 2 - 1, ambapo Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 43 kipindi cha kwanza kupitia kwa Jamal Mnyate, aliyeunganisha krosi ya Shiza kichuya.

Dakika mbili tu baada ya kuanza Kipindi cha pili, Tanzania Prisons, walisawazisha bao kupitia kwa Victor Hangaya, aliyemalizia krosi ya Salum Bosco ambaye leo ndiye alikuwa shujaa wa kumuangamiza mnyama na kupigia msumari wa mwisho katika dakika ya 64, akifunga kwa kichwa akiitendea haki pasi nzuri ya mpira wa adhabu uliopigwa na Mohamed Samatta

Kwa matokeo hayo, Simba SC inamaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 15, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 30 ambao nao kesho watashuka dimbani Uwanja wa Uhuru kukipiga na Ruvu Shooting.

Nao Azam Fc leo wameibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Mwadui Fc katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.

Katika mchezo huo Mwadui ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 30 kipindi cha kwanza kupitia kwa Hassan Kabunda.

Kabla ya kuingia bao hilo, mshambuliaji wa Mwadui Jerry Tegete dakika ya 19 alizua kizaazaa baada ya kufunga bao kwa mkono, ambalo lilikubaliwa na mwamuzi Enock Onoka, lakini baadaye alilikataa baada ya kushauriana na wasaidizi wake kufuatia wachezaji wa mabingwa hao kulilalamikia, jambo ambalo lilimfanya kuwalima kadi za njano Tegete na Abdallah Mfuko na kuamuru faulo ipigwe kuelekea lango la Mwadui.

Bao la kusawazisha la Azam FC lilifungwa na John Bocco dakika ya 54, bao la pili lilifungwa na Shaaban dakika ya 71 na la tatu Zekumbawira, dakika ya 74 na bao la kuhitimisha ushindi huo lilifungwa dakika ya 77 na Shaaban.
Ushindi huo unaifanya Azam FC kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi 25.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.