Habari za Punde

MUUNGANO WA WAPIGA KURA TANZANIA (TANVU) KUFANYA MATEMBEZI KUUNGA MKONO SERIKALI YA AWAMU YA TANO.

Mratibu Msaidizi na Katibu Mwenezi wa Habari na Mawasiliano wa Muungano wa Wapiga Kura Tanzania (TANVU) Bi.Berrynice Mayunga akizungumza na waandishi wa habari juu ya ya matembezi ya kuunga mkono Juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatakayoanzia Mkoani Singida Wilaya ya Ikungi hadi mkoani Dodoma kuanzia tarehe 26-30 Novemba, 2016.Kushoto ni Mkurugenzi wa Mipango na Uwezeshaji wa TANVU Bw.John Meena na Kushoto ni Mshauri wa chama hicho Bw.Donald Mathew.
************************************************************
Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Muungano wa Wapiga Kura Tanzania (TANVU) umeandaa matembezi ya kuunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatakayoanzia Mkoani Singida Wilaya ya Ikungi hadi mkoani Dodoma kuanzia tarehe 26-30 Novemba, 2016.

Hayo yamesemwa na Mratibu Msaidizi na Katibu Mwenezi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho Bi.Berrynice Mayunga wakati akiongea na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam.

Bi,Berrynice amesema kuwa sababu kubwa ya kufanya matembezi hayo ni kuipongeza Serikali kwa kuimarisha Utawala Bora kwa Uwajibikaji, Uwajibishaji, Uwazi, Maadili, Nidhamu kwa watumishi wa umma,kujenga dhamira ya kweli na Serikali kuhamia Dodoma.

Mengine ni pamoja na kujenga na kudumisha uzalendo ndani ya mioyo ya watanzania, ujengaji wa mfumo imara wa utawala bora,ujengaji wa misingi endelevu ya uchumi wa kati na ujengaji wa misingi na mfumo bora wa Tanzania ya Viwanda.

“Katika matembezi haya tunatarajia kushirikisha watanzania wazalendo zaidi ya 600 na kutakuwa na upandaji wa miti 12500 ikiwa ni kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwani imefanya mengi katika kipindi cha mwaka mmoja na watanzania wanaendelea kumpongeza na kumuunga mkono,” Alisema Bi Berrynice.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Uwezeshaji Muungano wa Wapiga Kura Tanzania (TANVU) Bw.John Meena ametoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi katika matembezi hayo na kupanda miti mkoani Dodoma ili kuupendezesha na kuufanya mji huo kuwa wa kijani.

Aidha ametoa rai kwa waandishi wa habari kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli na kueneza taarifa sahihi zenye kujenga na kuleta maendeleo nchini.

Matembezi haya yatashirikisha watu wanne kutoka kila mkoa nchini kutoka Muungano wa wapiga kura Tanzania (TANVU) pamoja na watanzania wote wanakaribishwa katika kushiriki matembezi haya.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.