Habari za Punde

MWAKA MMOJA WA RAIS DKT. MAGUFULI NA MAFANIKIO YA WIZARA YA HABARI

Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Mwenye macho haambiwi tazama na anayeshindwa kushukuru kwa jambo dogo hata akifanyiwa jambo kubwa kwake yeye ataliona dogo kwa sababu amedhamiria kutokuwa na roho ya kuridhika.

Novemba Tano mwaka 2016 ni mwaka mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipoapishwa kuwa Rais na Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Nchi hii ambapo ameweza kufanya mambo makubwa kiasi kwamba ukipingana na hali halisi basi utaonekana kuwa mtu usiyekuwa na shukrani kwa kila jambo.

Hatua hii inaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake toka aingie madarakani amekua mstari wa mbele kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana katika sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia viongozi wanaosimamia sekta hizo pamoja na serikali kwa ujumla.

Baada ya kuapishwa kwake Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano aliona umuhimu wa sekta ya Sanaa hivyo kuamua kuiundia Idara ili sekta hiyo iweze kusimamia kwa karibu kazi za Sanaa na kuwafanya wasanii kupata haki halali kupitia kazi za zao.

Katika hali ambayo haikutarajiwa na watu wengi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye hakusita kufanya ziara ya kushtukiza kwa wafanyabiashara wa kazi za Sanaa maeneo ya Soko la Kariakoo akiwa na lengo la kuwafichua wafanyabiashara wote wa kazi za Filamu na Muziki ambazo hazina stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinazoashiria uhaliali wa kazi hizo. 

Mhe. Nnauye anasema kuwa, hatua hii ni ya mwanzo kwa kuwaonyesha kuwa agizo la Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kulipa kodi kwa bidhaa zote zilizopo sokoni pamoja na kununua bidhaa halisi kwa kudai risiti linasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.

Ili kuua soko haramu la kazi za filamu na muziki wito kwa watanzania ulitolewa na Mhe. Nnauye kuwa tuwe na tabia ya uzalendo kwa kununua bidhaa za filamu zenye stampu ya TRA ili kusaidia katika kukusanya kodi na kuinua uchumi wa nchi lakini pia kuinua kipato cha wasanii.

Sanjari na hilo Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imedhamiria pia kurasimisha kazi ya sanaa kuwa shughuli rasmi ya kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano ya uongo wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Ili kuwezesha hilo Mhe. Nnauye amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano ya kuibua vipaji vya sanaa huku akiahidi kuendeleza sekta ya sanaa nchini ili kuwezesha vijana wengi kutambua vipaji vyao na kuweza kujiajiri na kuajiri wengine kupitia kazi za sanaa.

Wakale uneni msina kwao mtumwa. Lugha aushi na adhimu ya Kiswahili imeongeza mawanda mapya ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano ambapo Bunge la Afrika Mashariki (EALA) limekubali hoja ya kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika shughuli za bunge la Afrika Mashariki hatua hiyo dhahiri inayounga mkono pendekezo la mwenyekiti wa wakuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumzia hoja hiyo Mbunge wa EALA Mhe. Shayrose Banji amekiri Bunge la Afrika Mashariki limekubali kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi lakini haswa kuienzi na kuithamini lugha hii ambayo ndiyo pekee inayozungumzwa katika nchi zote za Jumuiya na hata nchi zilizo nje ya Jumuiya. 

Aidha, Mbunge wa EALA kutoka Tanzania Mhe. Adam Kimbisa amesema kuwa hapa Tanzania Kiswahili kinatumika kwa asilimia zaidi ya 95, Kenya zaidi ya asilimia 80, Uganda zaidi ya asilimia 50, Rwanda zaidi ya asilimia 50 na Burundi zaidi ya asilimia 60 hivyo ni wakati muafaka kwa Bunge hilo kuridhia lugha hii kuwa rasmi ndani ya Bunge.

Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza lugha ya Kiswahili, Kanisa Katoliki nchini liliandaa Kamusi ya Ukristo iliyoandikwa na Padre Jordan Nyenyembe na kuzinduliwa rasmi na Serikali mwezi Agosti mwaka 2016. Uzinduzi wa Kamusi hiyo utasaidia siyo tu uelewa wa imani na kukua kwa lugha ya Kiswahili, bali pia kuchochea upendo na amani nchini kwa kutumia lugha ya Kiswahili iliyopo ndani ya kamusi hiyo.

Dhahiri Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa kukutana na manguli, majagina na mangwiji, wakongwe na wapenzi wa lugha ya Kiswahili kujadili changamoto zinazoikabili tasnia ya lugha ya Kiswahili nchini na kupendekeza jinsi ya kuzitatua changamoto hizo katika kukubali na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuishadidisha lugha adhimu ya Kiswahili. Chambilecho cha Hayati Shaaban Robert alisema maajabu makuu mawili sintayasahau “Ni Mwalimu Nyerere na Lugha ya Kiswahili”

Aidha Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia James Wambura alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imezingatia umuhimu mkubwa wa kuwa na Sera ya Lugha ambayo ni mwongozo thabiti unaosimamia masuala yote yanayohusu Lugha nchini ambapo kwa sasa Wizara inaendelea na mchakato wa uandaaji wa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Lugha iliyofikia hatua ya ukusanyaji wa maoni ya awali ya wadau wa Lugha kwani tangu tulipopata uhuru mwaka 1961 masuala yahusuyo lugha katika nchi yetu yamezingatiwa kama kipengele muhimu katika Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997.

Pamoja na hayo katika kipindi cha mwaka mmoja sekta ya habari imepata manufaa kwa upande wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambapo Mhe. Nnauye ameutaka uongozi wa Shirika hilo kurejea mkataba wao na Kampuni ya Startimes wanayoshirikiana nao baada ya kubainika kuwepo na upungufu hivyo kuufanyia marekebisho mkataba huo ili kusaidia TBC kuboresha mapato tofauti na ilivyokuwa awali.

Aidha waziri huyo mwenye dhamana na masuala ya Habari alizungumza na uongozi wa juu wa Startimes na kuwataka kutekeleza maazimio ya mkataba wa awali wa kukamilisha ujenzi wa jengo la TBC pamoja na kuboresha studio ya shirika hilo kuifanya kuwa studio ya kisasa zaidi.

Sambamba na hayo uongozi huo wa Startimes umeridhia kuanza kufanya mafunzo ya kubadilishana uzoefu na wafanyakazi wa TBC kwa lengo la kuwaongezea ufanisi katika kutekeleza kazi zao kupitia mifumo ya teknolojia ya kisasa.

Katika kuleta maendeleo ya sekta ya habari serikali imekamilisha ndoto ya wanatansia wa habari kwa kuwaletea Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 uliokuwa ukisubiriwa kwa zaidi ya miaka ishirini, ambapo Muswada huo umelenga kuirasimisha sekta hiyo na kuifanya iweze kuheshimiwa kama tansia nyingine tofauti na ilivyo sasa.

Muswada huo umesheheni mambo mengi mazuri yatakayoweza kuinyanyua sekta hiyo ikiwemo kuanzishwa kwa Baraza Huru la Habari ambalo litakuwa likisimamia waandishi wote wa habari kwa kuwasajili, pia muswada utasaidia kuundwa kwa bodi ya ithibati ambapo bodi hiyo itakuwa ikitoa vitambulisho vya waandishi wa habari na kuishauri serikali katika mambo ya elimu ya mafunzo ya wanahabari.

Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha mwaka mmoja imeanzisha mfumo wa tiketi za elektroniki katika uwanja wa Taifa ikiwa na lengo la kuongeza mapato lakini pia kukidhi huduma ya haraka kwa wananchi wote watakaotumia Uwanja wa Taifa katika matukio mbalimbali ya michezo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mfumo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa mfumo wa elektroniki katika Uwanja wa Taifa ni wa kisasa na unawawezesha watu wote kuingia uwanjani ndani ya dakika 180 hivyo kuokoa muda wakati wa kuingia uwanjani.

Prof.Gabriel amesema kuwa kila mashine inatumia sekunde mbili kumruhusu mteja kuingia uwanjani tofauti na awali ambapo ilimlazimu mteja kupanga foleni kwa kutumia tiketi za kawaida wakati wa kuingia uwanjani lakini pia mfumo huo ni kichocheo kikubwa katika kuongeza mapato ya Serikali.

Rais huyu wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kuonyesha umuhimu wa michezo nchini ameweza kufanya mazungumzo mazuri na Mfalme Mohammed VI wa Morocco ambapo mazungumzo hayo yakaleta neema ya kujengewa uwanja wa mpira wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 80 (zaidi ya shilingi Bilioni 160) katika Mji wa Dodoma utakaokuwa mkubwa kuliko Uwanja wa Taifa uliopo Jijini Dar es Salaam. 

Heko Rais wetu, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, heko viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kufanya mambo makubwa na mazuri katika kila sekta ndani ya mwaka mmoja. Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali ya awamu ya tano ipo kwa ajili ya kuujenga uchumi wa nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu Mbariki Rais wetu, Mungu wabariki viongozi wote wa Serikali ya Awamu ya Tano. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.