Habari za Punde

PAC YAISHAURI SERIKALI KUANZISHA MFUKO WA UWEKEZAJI.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri Serikali kuanzisha mfumo maalum wa uwekezaji ili fedha zitakazowekwa katika mfuko huo zitumike kama mtaji katika maeneo ambayo nchi inataka kuwekeza.

Ushauri huo umetolewa mjini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo iliyochambuliwa kwa kina juu ya changamoto, maombi na mapendekezo yatakayoiwezesha nchi kusonga mbele.

Mwenyekiti Mhe. Kaboyoka amesema kuwa ushauri huo umetolewa baada ya kukwama kwa baadhi ya miradi pamoja na shughuli nyingine za Serikali zinazofanywa ili kuwasaidia wananchi kutokana na ukosefu wa fedha za kufanyia shughuli hizo hivyo kuanzishwa kwa mfuko huo kutahakikisha faida ya uwekezaji inaonekana.
“Sisi kama kamati tunaishauri Serikali kuanzisha mfuko maalum wa uwekezaji kwani utaisaidia Serikali kupata fedha za kufanyia maendeleo na kupata mitaji ya kuwekeza sehemu mbalimbali ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa na watanzania wanaiona faida ya uwekezaji”, alisema Mhe. Kaboyoka.

Mhe. Kaboyoka aliongeza kuwa kamati hiyo imependekeza kuwa mfuko huo uanzishwe chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kutumia mfumo wa kubakisha mapato kwa sababu ofisi hiyo ndiyo ina mamlaka ya kugawa fedha za Serikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Aidha, taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali imebaini kuwa pamoja na kuwa Idara ya Uhamiaji imeweka usimamizi wa utoaji wa viza katika Makao Makuu ya Idara, kwenye Balozi pamoja na maeneo ya mipaka ya nchi lakini mfumo wa kutoa viza kwa wageni wanaowasili nchini hauna mawasiliano mazuri.

Kukosekana kwa mawasiliano hayo kunasababisha mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali yanayotakiwa kukusanywa kutokana na utoaji wa viza hivyo kamati pia imeiomba Serikali kukamilisha haraka mradi wa Uhamiaji Mtandao (E- Migration) ili kuboresha njia za ukusanyaji wa mapato katika Idara hiyo.

Kwa upande wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyowasilishwa Bungeni hapo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vedasto Ngombale Mwiru ambaye ameelezea matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma katika Serikali za Mitaa pamoja na ushauri wa kamati hiyo katika kuhakikisha tatizo hilo linakoma.

Mhe. Ngombale Mwiru ameeleza kuwa Kamati imebaini udhaifu wa watendaji wa Halmashauri mbalimbali nchini katika usimamizi wa mikataba ya utekelezaji wa maendeleo unaopelekea miradi hiyo kuchelewa kukamilika, kukamilika kwa kiwango cha chini au kutokukamilika kabisa.

“Kulingana na taarifa hiyo, kamati imezishauri Halmashauri zote nchini kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake kusimamia miradi hiyo kwa ukaribu ili iweze kukamilika kwa wakati na kutumika kama ilivyo kusudiwa”, alisema Mhe.Ngombale Mwiru.

Ameongeza kuwa kumekuwa na tatizo katika Halmashauri hizo la kutotenga asilimia 10 ya fedha za mapato kutoka katika vyanzo vya ndani kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana ambapo kuna baadhi ya Halmashauri hazijawasilisha michango hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kutokana na tatizo hilo, Kamati imetoa agizo kwa Halmashauri zote kuandika barua ya kuthibitisha kulipa madeni hayo pia kuelezea mipango watakayotumia katika kutekeleza ulipaji huo.

Pia Kamati imeishauri Serikali kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya wanawake na vijana ili iwe sheria ambayo itatekelezwa kwa lazima hivyo kuendelea kuinua maisha ya wanawake na vijana kama ilivyokusudiwa.

Baada ya kamati zote mbili kuwasilisha taarifa hizo mbele ya Bunge,sasa ni zamu ya wabunge kujadili kwa kina masuala yaliyozungumziwa katika taarifa hizo kwa kutoa maoni yao na kuishauri Serikali kuhusu mapungufu yaliyojitokeza katika matumizi ya fedha kwa kuyapatia ufumbuzi ili yasijirudie katika taarifa zijazo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.