Habari za Punde

RAIS WA TFF JAMAL MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA MZEE SAMWEL SITTA, SHEIKH SAID MOHAMED

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kutokana na kifo cha Spika Mstaafu wa bunge hilo la Tanzania, Samwel Sitta.
Mzee Sitta ambaye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Urambo lililopo mkoani Tabora amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 7, 2016 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Technical iliyopo Munich nchini Ujerumani usiku wa kuamkia leo Novemba 7, 2016.

Rais Malinzi amesema kwamba Sitta ameacha alama ya ucheshi na upenzi katika michezo hususani soka kwani enzi zake hakuficha mapenzi yake kwa klabu ya Simba alikokuwa mwanachama.

Salamu za rambirambi za Rais Malinzi zimekwenda pia kwa Rais wa Klabu ya Simba, Evance Aveva, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki. Amewataka kuwa watulivu wakati huu mgumu wa kumpoteza Mzee Samwel Sitta na kwamba anaungana nao kwenye maombolezo.

Akimwelezea zaidi Mzee Sitta, Rais Malinzi amesema kwamba "Binafsi nitamkumbuka na kuenzi uchapakazi wake. Alikuwa Mwanamichezo aliyekuwa na Mzalendo hususani alipokuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na alikuwa pia Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba. Aliwahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali kwa vipindi tofauti. 

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina la Bwana Lihimidiwe.
**********************************

MALINZI AMLILIA SHEIKH SAID MOHAMMED WA AZAM
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh Said Muhammad aliyefariki dunia leo Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Taarifa za kufariki dunia kwa Mzee Said Muhammad ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi zimethibitishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba aliyesema kwamba alifariki dunia katika wodi ya Wagonjwa mahututi (ICU) hospitalini hapo baada ya kuzidiwa ghafla nyumbani kwake.

Kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Yahya Mohammed, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, Uongozi wa Klabu ya Azam, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki. Amewataka kuwa watulivu wakati huu mgumu wa kumpoteza Mzee Said Muhammad.

Katika salamu zake, Malinzi amemwelezea marehemu Said Muhammad kuwa alikuwa hazina katika mpira wa miguu nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mchango ya mawazo na miongozo katika Kamati ya Utendaji ya TFF. 

Aliongoza Klabu ya Azam kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe.

“Ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Mzee Muhammad ndiye aliyekuwa na umri mkubwa ukilinganisha na wajumbe wengine, lakini alikuwa hakosi vikao muhimu. Mchango wake wa mawazo ulikuwa nguzo kwetu. Nimepokea taarifa hizi za kifo chake kwa masikitiko makubwa,” amesema Rais Malinzi leo mara baada ya kupokea taarifa za kifo hicho.

Taratibu za mazishi zinafanywa nyumbani kwa marehemu. Sheikh Said Muhammad atazikwa kesho Jumanne alasiri  katika makaburi ya Kisutu baada ya mwili wake kuswaliwa msikiti wa Maamur ulioko Upanga, jijini Dar es Salaam.

Inna lillah wainna ilayh  Rajiuun.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.