Habari za Punde

SHILINGI BILIONI 3 KUKARABATI MAGEREZA NCHINI

                            Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3 katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kukarabati, kupanua na kumalizia ujenzi wa mabweni mapya pamoja na majengo ya utawala katika baadhi ya magereza nchini.  
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ameyathibitisha hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Hawa Mwaifunga (Mbunge wa Viti Maalumu) lililohoji kuhusu mpango wa Serikali katika kuhakikisha hali za magereza katika Mkoa wa Tabora zinaboreshwa.
Mhe. Mwigulu amesema kuwa katika kuhakikisha hali ya magereza nchini inaboreshwa ili kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa, Serikali inaendelea na mpango endelevu wa kufanya upanuzi wa magereza ya zamani na kujenga magereza mapya katika kila Wilaya ambapo utekelezaji huo unafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga bilioni 3 katika Bajeti kupitia Fungu la Maendeleo kwa ajili ya kukarabati magereza ambapo shilingi milioni 185 kati ya bajeti iliyotengwa ni kwa ajili ya kukarabati magereza ya Mkoa wa Tabora, hivyo tunategemea magereza ya mkoa huo yatakuwa katika hali nzuri”, amesema Mwigulu.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua msongamano wa mahabusu uliopo katika magereza mengi nchini na kuongeza kuwa Jukwaa la Haki Jinai limekuwa likifanya vikao vya kuharakisha kesi ambazo upelelezi wake haujakamilika ili kupunguza msongamano huo.
Aidha, Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali inahakikisha Askari Wapelelezi wanapewa mafunzo kulingana na kazi yao ili waweze kufanya ukamataji wa watuhumiwa kwa kuzingatia uzito wa ushahidi wa muhusika na kuepusha malalamiko ya kubambikiwa kesi na kujikuta Serikali inatumia gharama nyingi kuwatunza mahabusu hao.
Kuhusu usalama wa askari, Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi nchini kwa kuwapa vitendea kazi bora na kuwajengea uwezo wa mafunzo askari hao ili waweze kukabiliana na matukio ya uhalifu dhidi ya wanananchi na mali zao pamoja na uvamizi wa vituo vya polisi nchini.
“Hadi kufikia Septemba 2016 Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha 19 kati ya 23 zilizoporwa kutoka kwa askari waliovamiwa wakiwa wakitekeleza majukumu yao hatua inayoonesha jeshi la Polisi linavyofanya kazi kwa umakini” alisema Mwigulu.

Kwa upande mwingine, Waziri Mwigulu ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa katika vituo vya Polisi vilivyo karibu pindi wanapokuwa na shaka juu ya watu wasiowatambua au kufanya kazi zisizoeleweka ili kuwahakikishia wananchi usalama wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo.     

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.