Habari za Punde

TRA YATAKIWA KUWA MAKINI NA WANAOINGIZA NGUO NCHINI BILA YA KULIPIA KODI.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kushoto akipata maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni inayotengeneza batiki na unyonyaji wa maji taka Genevive Investment Bi. Jane Mwaituka kulia alipotembelea banda lao wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya biashara na wajasiliamari wanawake jijini Dar es salaam.
********************************************
Na Ally Daud-MAELEZO. 
MAMLAKA ya mapato nchini (TRA) imetakiwa kuwa makini na wafanyabiashara wanaoingiza nguo nchini bila ya kulipa kodi kwa kuwa hawalipii biashara zao kwa kila mzigo unaoingia hivyo kuchangia kuleta hasara ukusanyaji wa pato la taifa. 

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage wakati wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya ujasiriamali kwa wanawake yaliyofanyika jijini Dar es salaam yakiwa na lengo la kukuza na kuwezesha wanawake kujitegemea kiuchumi na kukuza maendeleo ya taifa kupitia viwanda. 

“Napenda kuwaambia TRA wawe makini wafanyabiashara wanaoingiza nguo nchini bila ya kulipa kodi kwa kuwa hawalipii biashara zao kwa kila mzigo unaoingia hivyo kuchangia kuleta hasara katika pato la taifa kwa kupoteza takribani shilingi bilioni 319 kutokana ukwepaji wa kodi za nguo zinazoingia nchini” alisema Waziri Mwijage.

Aidha Waziri Mwijage amesema kuwa kwa kufanya hivyo TRA itaweza kukusanya mapato mengi zaidi na kukuza uchumi wa nchi kupitia ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara na wanaostahili kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi. 

Mbali na hayo Waziri Mwijage amesema kuwa wanawake wajasiriamali wanatakiwa kuwa wabunifu na sio kuiga ubunifu wa mtu mwingine kwa asilimia kubwa ili kuweza kujiletea masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi ili kujipatia soko la kimataifa. 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa MOWE Bi. Elihaika Mrema amesema kuwa maonyesho hayo yamewalenga wanawake wajasiriamali kuonyesha na kuuza bidhaa zao ambazo zimetokana na ubunifu wao kwa maendeleo ya mwanammke na Tanzania kwa ujumla ili kukuza pato la taifa. 

“Wanawake wajasiriamali wanatakiwa wawe wabunifu katika kubuni biashara mbalimbali za kujikwamua na uchumi ili kuacha kutegemea wanaume kwa asilimia kubwa na kuendesha jamii kubwa ya Tanzania” alisema Bi. Elihaika.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kulia akisalimiana na Meneja wa huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA Bw. Gabriel Mwangosi katikati alipotembelea banda lao wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya biashara na wajasiliamari wanawake jijini Dar es salaam,kushoto ni Meneja wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi Bi. Valentina Baltazar.
Afisa Elimu Mkuu kwa mlipa kodi wa TRA Bi. Rose Mahendeka akiwapa maelekezo wateja waliotembelea banda hilo wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya biashara na wajasiliamari wanawake jijini Dar es salaam. 
Picha Na Ally Daud- MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.