Habari za Punde

VUAI AFUNGUA MAFUNZO YA WATUMISHI WA CCM Z'BAR

NA MWANDISHI WETU,  ZANZIBAR.                           
  Chama Cha Mapinduzi kimewataka Watumishi wake kuelekeza nguvu zaidi katika kutekeleza ipasavyo majukumu yao kwa weledi na juhudi kubwa ili kukiletea ufanisi ndani ya Chama hicho.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Vuai Ali Vuai, ametoa kauli hiyo, alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya  watumishi wa Chama na Jumuiya zake wa kada ya Udereva, Walinzi, Waangalizi wa Ofisi, Makarani wa Masjala na Wahudumu wa Chama hicho, kutoka Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar. Mafunzo hayo ya takriban wiki moja yanafanyika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, Mjini Unguja.

Amesema Chama Cha Mapinduzi kinaridhishwa na utendaji wa watumishi wa kada hizo, isipokuwa  CCM kimeona kuna umuhimu wa kuandaa mafunzo maalum kwa watumishi hao, kwa lengo la kuwajengea uwezo na uelewa mpana zaidi katika kufanikisha majukumu yao na hivyo waendane na kasi ya Chama kwa sasa.

Mhe. Vuai amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwapatia mafunzo watumishi wake wa kada mbali mbali kwa lengo sio tu la kuwaleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Chama bali pia kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu mbadala za kiutumishi.

“Chama Cha Mapinduzi kitafanya kila linalowezeka kuhakikisha watumishi wake wa ngazi zote wanapatiwa mafunzo pamoja na kuwaendeleza kielimu,  kwa madhumuni ya kunyanyua viwango vyao vya uelewa, na hivyo kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi”. Alidai Mhe. Vuai.

Amesisitiza haja kwa wanafunzo hao juu ya umuhimu wa kuimarisha Chama  na kudumisha suala zima la nidhamu pamoja na kuwepo kwa mawasiliano mazuri baina yao na Viongozi wao, ni dhahiri kutakijengea heshima kubwa chama hicho mbele ya jamii.

Nao wanafunzo hao, wametumia mkutano huo kumpongeza kwa dhati Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa jinsi anavyotekeleza kwa kasi kubwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 pamoja na kupambana vilivyo na suala zima la rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake.

Wamempongeza pia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed  Shein, kwa kusimamia vyema Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 - 2020, kusimamia suala zima la amani na utulivu wa nchi, kuimarisha huduma za kijamii na miundombinu ya kiuchumi kwa maslahi ya Wananchi wa Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.