Habari za Punde

WABUNGE WAPEWA SEMINA KUHUSU MKATABA WA EPA

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepewa semina kuhusu Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya (EPA) ili wapate uelewa na hatimaye kuishauri Serikali juu ya suala hilo.

Semina hiyo imetolewa kwa Wabunge leo mjini Dodoma na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Saalam akiwemo Prof. Palamagamba Kabudi, Dkt. Ng’waza Kamata na Dkt. John Jingu pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda. 

Akifungua semina hiyo, Spika Mhe. Job Ndugai amesema kuwa anatambua umuhimu wa mkataba huo ni vema Wabunge watumie fursa ya semina hiyo ili watakapofika kwenye mjadala wenyewe ndani ya Bunge wawe na uelewa mpana kwa manufaa ya nchi.

“Natambua kwamba majadiliano haya yamefanyika sana hasa katika vikao vya Bunge lililopita, lakini kwa kuwa wabunge wengi ni wapya tumeona kuna umuhimu wa kuandaa Semina hii ili tuweze kupata elimu na kuongeza uelewa wa jambo hili kabla ya kuujadili rasmi ndani ya Bunge letu”, alisema Ndugai.

Ameongeza kuwa semina hii pia itawapa wabunge nafasi ya kuuliza maswali na kufanya majadiliano ya jumla ili kupata ufafanuzi wa kina juu ya mambo mbalimbali yanayohusu mkataba huo, hiyo yote ikiwa ni njia ya kuwaelimisha ili siku ya majadiliano rasmi watoe mapendekezo yatakayoleta tija na manufaa kwa nchi yetu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda alipokuwa akiwasilisha mada juu ya chimbuko, mustakabali na uchambuzi wa EPA amesema hiyo ni namna bora ya kuwashirikisha na kuwapa uelewa Wabunge ili waweze kujadili mkataba huo kwa manufaa ya taifa. 

Nao wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamewashauri wabunge kutumia semina hiyo kama muongozo utakaowawezesha kuboresha mjadala wao wakati wa kutoa michango yao ndani ya Bunge ili waweze kutoa majibu sahihi siku ya kuujadili mkataba huo.

Mswada huo unatarajiwa kuwasililishwa Bungeni Novemba 10 mwaka huu ambapo mjadala huo utapelekea kuishauri Serikali kuhusu hatma ya mkataba huo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.