Habari za Punde

WAHITIMU CBE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA AJIRA KWA KUANZISHA VIWANDA VIDOGO VIDOGO

Mwenyekiti wa Bodi ya CBE Prof.Mathew Luhanga akizungumzana wahitimu wa Chuo hicho wakati wa Mahafali ya 51 jijini Dar es 
salaam.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. CharlesMwijage akizungumza na wahitimu 1,811 wa Chuo cha Elimu ya Biashara 
(CBE) waliotunukiwa stahili zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016 
wakati wa Mahafali ya 51 ya chuo jijini Dar es salaam.
Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara CBE wakivaa 
kofia zao mara baada ya kutunukiwa Shahada zao katika fani mbalimbali 
wakati wa mahafali ya 51 ya Chuo cha Elimu ya Biashara jijini Dar es 
salaam.
**************************************************
Na. Mwandishi Wetu - Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage
amewataka wahitimu 1,811 wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)
waliotunukiwa stahili zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016
kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini kwa kuanzisha makampuni na
viwanda vidogo vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.

Akizungumza katika mahafali ya 51 ya chuo hicho jijini Dar es salaam
Mhe.Mwijage amesema kuwa makampuni na viwanda vidogo vidogo
watakavyoanzisha vitatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora
ambazo zitauzwa kote duniani hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuwapatia
ajira ya uhakika.

Amesema Serikali ya Tanzania inapenda kuwaona Wawekezaji wengi wa
Kitanzania wakiingia na kuwekeza kwenye rasilimali mbalimbali
zilizopo nchini Tanzania badala ya kuwaachia wageni kwa kuwa inao
wasomi waliobobea kwenye fani ya biashara pamoja na ujasiriamali.

" Taifa letu limebarikiwa kuwa na fursa nyingi za kujiletea maendeleo,
Serikali ingependa kuona wawekezaji wengi wa Kitanzania wakiwekeza
kwenye rasilimali zilizopo kwa mfano tunayo gesi, madini, kilimo na na
rasilimali nyinginezo nyingi" Amesisitiza Mhe.Mwijage.

Amefafanua kuwa Serikali itaendelaea kuwekeza kwenye Elimu ya Biashara
kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiajiri na kuajiriwa katika sekta
binafsi hasa Biashara.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na mikakati ya kudumisha
ushirikiano na nchi za jirani kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa
lengo la kuondoa kuondoa vikwazo mbalimbali vya kiuchumi, kijamii na
kibiashara katika nchi zilizo katika ukanda huo ili kuwawezesha
watanzania kuendelea kunufaika.

" Nawaomba sana muondoe hofu mzitumie fursa zilizoko nje ya Tanzania,
msifungwe na mipaka , fuateni taratibu zilizopo ili mjinufaishe na
kulinufaisha Taifa letu" Amebainisha Mhe.Mwijage.

Katika hatua nyingine amekipongeza chuo hicho na wake kwa kuendelea
kupanua wigo wa utoaji wa elimu katika fani mbalimbali kwa kuongeza
matawi ya chuo hicho kwenye mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya na
kukiwezesha kuwa na kufikisha idadi ya wanachuo wapatao 11,000.

Aidha, amesema kuwa ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya wanachuo
wanaodahiliwa kila mwaka na changamoto ya uhaba wa majengo na kumbi za
mihadhara amewataka viongozi na watendaji wa Wizara yake washirikiane
na Bodi ya CBE na Menejimenti ya chuo hicho kuangalia uwezekano wa
kujenga majengo makubwa na marefu katika eneo la chuo hicho ili
kukidhi mahitaji ya miundombinu.

" Ili kufanikisha hili Serikali tutasaidia kutenga fedha pia kuwa na
jukumu la kutafuta wabia na Serikali tutatafuta udhamini wa ubia huo"
Amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof.Emanuel
Mjema akizungumza wakati wa mahafali hayo ameeleza kuwa chuo
anachokisimamia kimeweza kutoa wahitimu kwenye mafunzo ya biashara
nyanja za Uhasibu , Usimamizi wa Biashara, Usimamizi wa Masoko ,
Ununuzi na Ugavi , Mizani na Vipimo ,TEHAMA pamoja na mafunzo ya
Shahada ya Ualimu katika Biashara.

Amesema kuwa mafunzo hayo yamewanufaisha Watanzania kwa kuwawezesha
ujiajiri na kuajiriwa na kuongeza kuwa chuo hicho hivi karibuni
kimeanzisha Shahada mbili za Uzamili katika fani za Habari na
Mawasiliano.

Prof.Mjema ameeleza kuwa chuo hicho kina wahadhiri waliobobea katika
nyanja mbalimbali za mambo ya Elimu ya Biashara na wanao uwezo wa
kufanya tafiti na kutoa ushauri katika nyanja ya biashara na kuiomba
Serikali kuwatumia wataalam hao.

" CBE tunao wataalam waliobobea katika nyanja ya Biasahara na tuna
uwezo wa kufanya tafiti na kutoa ushauri katika shughuli mbalimbali ,
ni wakati muafaka Serikali itutumie hasa wakati huu tunapoelekea
kwenye ujenzi wa Tanzania ya viwanda ili tuwezesha kutoa taarifa
sahihi za Biashara na uwekezaji" Amesisitiza Prof.Mjema.

Amesisitiza kuwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimekuwa ni Taasisi
ya kwanza ya Elimu ya juu kufanya Utafiti na kuendesha Kongamano juu
ya Fursa za Kibiashara na Uwekezaji zilizopo mjini Dodoma, kongamano
ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini fursa za Biashara na
uwekezaji pamoja na namna bora na endelevu ya kuzitumia fursa hizo.

Kwa upande wao baadhi ya wahitimu wa chuo hicho waliohudhuria mahafali
hayo wakizungumza kwa nyakati mbalimbali wamesema kuwa wako tayari
kulitumikia taifa kwa kuwa wanao uwezo na ujuzi wa kutekeleza majukumu
yao kikamilifu.

Wameeleza kuwa licha ya changamoto ya uhaba wa nafasi za ajira
Serikali wako tayari kujiajiri wenyewe kwa kuanzisha makampuni yao
wenyewe yatakayowawezesha kujiajiri wenyewe na kuajiri vijana wengine
kwa kuitumia elimu waliyoipata chuoni hapo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.