Habari za Punde

WAJASIRIAMALI KIGOMA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA TPSF

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Yuda Thadeus Mboya (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wajasiriamali iliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (Tanzania Private Sector Foundation),(Kulia) Meneja wa SIDO mkoa Kigoma, Gervas Ntahamba na (wa pili kushoto) Mwenyekiti wa chama cha Wafanyabiashara na wenye viwanda mkoa Kigoma (TCCIA), Ramadhani Gange. 
Mwenyekiti wa chama cha Wafanyabiashara na wenye viwanda mkoa Kigoma (TCCIA), Ramadhani Gange (wa pili kushoto aliyesimama) akitoa neno la shukrani kwa mgeni Rasmi wakati wa ufunguzi wa semina kwa wajasiliamali iliyotayarishwa na taasisi ya sekta binafasi Tanzania (TPSF)
Baadhi ya wajasiliamali wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wakijadiliana mada mbalimbali zilizotolewa na wawezeshaji wakati wa semina ya wajasiriamali iliyoandaliwa na taasisi ya sekta binafasi Tanzania (TPSF).
**************************************
Wajasiriamali waliopo mkoani Kigoma wametakiwa kutumia raslimali mbalimbali zilizopo mkoani humo na fursa zinazojitokeza kwa sasa kuibua miradi ya biashara na kuendesha biashara yao kitaalamu wakiwa na malengo ya kujikwamua kutoka katika hali ya umaskini. 

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji , Yuda Thadeus Mboya, wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu ya mbinu za kuendeleza wajasiriamali yaliyoandaliwa na taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na kufanyika katika ukumbi wa St.Martha mjini Kigoma. 

Alisema serikali imefungua milango ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kwa kutumia fursa zilizopo hivyo aliwataka kushiriki mafunzo mbalimbali ya mbinu za biashara na kuibua miradi ya biashara na kuwa na utayari wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika biashara kwa kipindi hiki mojawapo ikiwa ni ushindani mkubwa na kufanya biashara kwa kufuata njia halali zinazotakiwa ikiwemo kulipa kodi za serikali kwa mujibu wa sheria. 

“Hivi sasa biashara zinafanyika katika mazingira ya ushindani na wateja wanahitaji bidhaa zenye ubora hivyo haitakiwi ubabaishaji wa aina yoyote kwa mfanyabiashara anayetaka mafanikio”.Alisema Mboya. 

Aliipongeza taasisi ya TPSF kwa kuendesha miradi ya mafunzo kwa wajasiariamali sehemu mbalimbali nchini “Nawapongeza kwa kuwafikishia mafunzo wajasiriamali wa ngazi za chini katika ngazi ya mikoa na wilaya kwa kuwa wafanyabiashara wakipata mafunzo kama haya kwa vyovyote wataweza kupata mafanikio katika shughuli zao”.Alisema . 

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Mafunzo kutoka taasisi ya TPSF,Celestine Mkama alisema kuwa taasisi hiyo inaendesha mradi wa kuwapatia mafunzo wajasiriamali kuhusiana na mbinu mbalimbali za kufanya biashara kwa lengo la kupata mafanikio. 

“Mafunzo haya yamelenga kuwapatia maarifa wafanyabiashara wadogo ili yawajengee uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo katika biashara “Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa wakikosa mbinu za kufanya biashara kutokana na kukosa elimu ya biashara ndio maana tumeona tuwasaidie katika eneo hili la kuwajengea uwezo kupitia kuwapatia elimu ya ujasiriamali”.Alisema Bw.Mkama. 

Mkama alisema baadhi ya masuala yanayofundishwa kupitia mafunzo haya ni utunzaji wa mahesabu ya biashara,nidhamu katika matumizi ya fedha,utunzaji wa kumbukumbu za biashara na jinsi ya kupanga miradi. Alisema mafunzo haya tayari yameishafanyika katika mikoa mbalimbali na kuwafikia wajasiriamali wengi na tathmini ya awali inaonyesha kuwa waliopata mafunzo haya wameanza kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kutoa mchango katika pato la taifa kupitia kulipa kodi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.