Habari za Punde

WATUHUMIWA VINARA WENGINE WATANO WA NYARA ZA SERIKALI WAPANDISHWA MAHAKAMANI

Hatimaye Vinara wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa kukusanya, kuuza vipande 50 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh. milioni 392.8 wamepandishwa katika mahakamani wakikabiliwa na mashtaka manne ya kuhujumu uchumi akiwamo, Yusuf Ali maarufu kama Shehe ama "Mpemba" (35).
Mbali na "Mpemba", washtakiwa wengine n mfanyabiashara mkazi wa Mrimba, Mkoani Morogoro, Charles Mrutu maarufu Mangi Mapikipiki ama Mangi Mpare (37), wakazi wa Dar es Salaam, Benedict Kungwa (40) Jumanne Chima maarufu Jizzo ama JK (30), Pius Kulagwa (46) na Dereva wa Vikindu, Pwani Ahmed Nyagongo (33).

Washtakiwa wote walisomewa mashtaka yao leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.Wakili wa Serikali Paul Kadushi, alidai kuwa kati ya Januari, mwaka 2014 na Oktoba, mwaka huu maeneo tofauti Mkoani Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara washtakiwa wakiwa na wenzao ambao bado hawajashtakiwa mahakamani, walijihusisha na matukio ya uhalifu.

Ilidaiwa pia, washtakiwa walijihusisha kukusanya, kuuza vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Kimarekani, 180,000 (sawa na Sh. 392,817,600) mali ya Serikali ya Tanzania, bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la pili, Oktoba 26, mwaka huu eneo la Mbagala Zakhem Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani, 30,000 (sawa na Sh. 65,469,600) mali ya Serikali ya Tanzania, bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Shtaka la tatu na la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 27 na 29, mwaka huu na eneo la Tabata Kisukulu, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa na vipande 40 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa kilo 69.56 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 150,000 (sawa na Sh. 327,348,000) mali ya Serikali ya Tanzania, bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Kadushi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba Jamhuri inaandaa nyaraka mbalimbali ikiwamo maelezo ya mashahidi pamoja na vilelezo kwa ajili ya kuwasilisha taarifa katika Mahakama Maalum ya kesi za Kuhujumu Uchumi na Rushwa (mafisadi).

Hakimu Simba alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi za kuhujumu uchumi.
Kesi hiyo itatajwa Desemba Mosi, mwaka huu na washtakiwa wamepelekwa mahabusu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.