Habari za Punde

WAZIRI MWIJAGE AWAPONGEZA TRA KWA JITIHADA ZA KUENDELEA KUELIMISHA WAFANYABIASHARA

Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage ameipongeza na kuishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa jitihada za kuendelea kuelimisha wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kulipa kodi utakaoiwezesha Serikali kusonga mbele katika suala zima na ukuzaji wa viwanda vya ndani hapa nchini.

Mhe. Mwijage aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa mwaka wa Taasisi isiyo ya kiserikali  inayotoa Msimbomilia (Barcode) za bidhaa (GS1); uliofanyika tarehe 29 Novemba 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya GS1 na TRA kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wadau wao, kujadili mambo muhimu ya kodi yanayohusu umuhimu wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika  kuweza kupata msimbomilia (barcodes 620) na kuweza kuzitambulisha bidhaa za Tanzania kimataifa pamoja na kuadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Waziri Mwijage aliliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha kila mfanyabiashara anayemiliki viwanda vidogo na vya kati kuhakikisha anakuwa  na TIN na namba ya msimbomilia 620 inayotolewa na GS1 Tanzania kabla ya kuhuisha vyeti vyao vya biashara.

Aidha  Waziri Mwijage amesema kuwa uchumi wa viwanda unatakiwa kukua nchini ili kuweza kuzalisha bidhaa bora zitakazouzwa ndani na nje ya nchi na  kukusanya kodi stahiki itakayoiwezesha Serikali kutoa huduma bora za kijamii  kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania .
“Ifike wakati wafanyabiashara muwaelewe vizuri TRA na kulipa kodi stahiki ya Serikali, ili nchi iweze kusonga mbele” alisema Mhe. Mwijage.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Bi. Rose Mahendeka alisema kuwa wafanyabiashara wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka msimbomilia (Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kabla ya kwenda kupata huduma ya msimbomilia 620.
Bi. Mahendeka aliwasisitiza wadau hao kuhakikisha wanajisajili na TIN na wale waliojisajili kuhakikisha wanahakiki taarifa zao ili kurahisisha upatikanaji wa Msimbomilia 620 na kuiwezesha TRA kupata takwimu sahihi za wafanyabiashara wazalishaji na wanaouza bidhaa zao nje ya nchi.
“Wafanyabiashara wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka Msimbomilia(Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi(TIN) kabla ya kwenda kupata huduma” alisisitiza Bi. Mahendeka.
Aidha Bi. Mahendeka alisema kuwa wafanyabiashara ambao wanahitaji kuuza bidhaa zao kwa kutumia msimbomilia wanapaswa kulipa kodi bila ya kukwepa ili kuiwezesha Tanzania kupiga hatua kufikia uchumi wa viwanda na vilevile kuweza kutoa huduma bora kwa maendeleo ya jamii.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya GS1 Bw. Gideon Mazara alitoa rai kwa wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa kutumia Msimbomilia 620 wa Tanzania na kuweza kutangaza bidhaa za hapa nchini ili kupata soko la kimataifa litakalowezesha nchi kufikia uchumi wa kati .

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.