Habari za Punde

WIZARA YA ELIMU YAKABIDHIWA RASMI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo, Jinsia , Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga wa kwanza kulia akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Bi. Maimuna  Tarish katikati hati za makubaliano ya kuhamishia Vyuo vya maendeleo ya Wananchi wakati wa hafla fupi ya makabidhiano hayo yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
 *****************************************
Na Ally Daud-MAELEZO.
WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imekabidhiwa rasmi Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vipatavyo 55 kutoka Wizara ya Maendeleo, Jinsia , Wazee na Watoto ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli alilotoa Aprili mwaka huu wakati akikabidhi hati idhini kwa Wizara hiyo ili kuendeleza vyuo hivyo nchini.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa makabidhiano ya nyaraka za makubaliano Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo, Jinsia , Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga amesema kuwa kukabdhiwa kwa vyuo hivyo kwenye Wizara ya Elimu ni utekelezaji wa Agizo la Mhe. Rais Magufuli la kuhamishia lililotolewa Aprili mwaka huu.
“Tumekabidhi rasmi vyuo vya maendeleo ya wananchi mikononi mwa wizara ya Elimu kama alivyotuagiza Mh. Rais Aprili mwaka huu ili visimamiwe kwa utaratibu mzuri pamoja na maendeleo yake kwa ajili ya wananchi na taifa kwa ujumla” alisema Bi. Nkinga.
Aidha Bi. Nkinga amesema kuwa vyuo hivyo vitaendelea na shughuli zake za kutoa elimu kwa wananchi kama ilivyokua zamani ikiwa chini ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kama ilivyoonyeshwa kwenye hati idhini iliyotolewa na Mh. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Bi. Maimuna Tarish amesema kuwa Vyuo hivyo vinatakiwa kuwa na ufundi stadi ambao upo kwenye viwango vya Wizara hiyo ili kufikia uchumi wa kati hususani kwenye viwanda.
“Vyuo sasa vinatakiwa kutoa mafundi na wahandisi wenye ufundi stadi ambao upo kwenye kiwango cha wizara ya Elimu ili kukidhi teknolojia na kukuza uchumi wan chi kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda” alisema Bi.Tarish.
Naye Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Arnautoglu Bi. Nsembia Mbwambo amesema kuwa wanaamini Wizara ya Elimu itawapa muongozo mzuri zaidi kuongeza ufundi stadi kwa wanafunzi wa vyuo hivyo.
Makabidhiano hayo yaliyofanywa na Wizara hizo mbili ni makubaliano ya utekelezaji wa agizo la Mh. Rais lililotolewa Aprili mwaka huu kuwa vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi viratibiwe na Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo, Jinsia , Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga aliyesimama akiongea na watendaji wa Wizara hiyo na Wizara ya Elimu hawapo pichani wakati wa makabidhiano ya nyaraka za makubaliano ya kuhamishia Vyuo vya maendeleo ya Wananchi Wizara ya Elimu yaliyofanyika jijini Dar es salaam. Aliyekaa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Bi. Maimuna  Tarish. Picha Na Ally Daud- MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.