Habari za Punde

YAHYA HAMAD APENDEKEZWA KUWA KAIMU MWENYEKITI KAMATI YA SAA 72 YA TFF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kunashukuru wanafamilia wa soka kwa salamu mbalimbali za rambirambi kutokana na msiba wa Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh Said Muhammad aliyefariki dunia Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Kutokana na kufariki kwa Sheikh Muhammed, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amempendekeza Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Bwana Yahya Hamad - kukaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji Ligi (Kamati ya Saa 72) ili kushughulia masuala yote ya mechi zilizochezwa tangu mwanzo wa Novemba, 2016 baada ya kifo cha Sheikh Muhammad.

Hayati Sheikh Said Muhammad kualikuwa hazina katika mpira wa miguu nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mchango ya mawazo na miongozo katika Kamati ya Utendaji ya TFF. 

Itakumbukwa kwamba Sheikh Muhammad aliongoza Klabu ya Azam kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe.

Tunachukua nafasi hii kutoa wito kwa klabu kumpa ushirikiano Bwana Hamad katika majukumu yake mapya akiongoza kamati hiyo yenye wajumbe ambao ni Baruan Muhuza (Azam Tv), Boniface Wambura (Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi), Jonas Kiwia (Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano TFF), Philemon Ntahilaja (Mdau wa Mpira wa Miguu), Charles Ndagala (Katibu Kamati ya Waamuzi ya TFF), Kanali Mstaafu wa JWTZ, Isaron Chacha na Steven Mnguto ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya ligi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.