Habari za Punde

BAADA YA MGOMO YANGA YAIBUKIA KWA NDANDA FC YAICHAPA MABAO 4-0


Wachezaji wa Yanga Simon Msuva (kushoto) na Amis Tambwe (kulia) wakimpongeza mwenzao Donald Ngoma baada ya kuifungia timya yao bao la pili kati ya manne yaliyofungwa dhidi ya Ndanda Fc katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huoYanga wameibuka na ushindi wa mabao 4-0, huku mabaomawili yakifungwa na Donald Ngoma, la tatu likifungwa na Amis Tambwe na la Nne likifungwa na Viceny Bossou.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo wamewafuta machungu mashabiki wao na kurejea katika mbio za kuwania ubingwa kwa tofauti ya Pointi moja na watazizao simba baada ya kuwachabanga Ndanda Fc kwa mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

Yanga wamefikisha pointi 40 wakiwa nafasi ya pili ambapo alama hizo zinaweza kuongezeka na kurudi nne za awali endapo Simba atashinda mchezo wake wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa uwanjani hapo.

Mashabiki wa timu hiyo waliwatolea maneno makali wachezaji wa mabingwa hao katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao moja dhidi ya African Lyon Ijumaa iliyopita kwa madai walifanya kusudi kupata matokeo hayo ili kushinikiza uongozi kuwalipa mishahara yao iliyochelewa mwezi Novemba.

Katika dakika 25 za kwanza Yanga walikuwa tayari wamefunga mabao matatu kupitia kwa Donald Ngoma aliyefunga mawili dakika ya tatu na 21 huku Amissi Tambwe akifunga la tatu na kuwafanya mabingwa hao kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-0.

Dakika ya 60 kocha Lwandamina alimuingiza kiungo Justine Zulu ambaye alionyesha umahiri mkubwa wa kupiga pasi na kukaba hali iliyoibua shangwe kila alipogusa mpira.

Beki Vicent Bossou aliifungia Yanga bao la nne dakika ya 88 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Juma Abdul.

Kocha wa Ndanda Hamimu Mawazo aliwapumzisha Salvatory Ntebe na Abuu Ubwa na kuwaingiza Ayoub Shabani pamoja na Salum Minely.

Kwa upande wa Yanga iliwatoa Saidi Makapu, Haruna Niyonzima na Emmanuel Martin nafasi zao zikachukuliwa na Zulu, Thaban Kamusoko pamoja na Deus Kaseke.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.