Habari za Punde

CCBRT KUONGOZA KAMPENI YA KUCHANGIA DAM MKOA WA DAR

 Kwa zaidi ya siku tatu, Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) – kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa Damu Salama, Timu ya menejmenti ya afya ya mkoa wa Dar es Salaam na Lions Platinum of Dar es Salaam wameendesha kampeni maalumu kukusanya damu inayohitajika katika kipindi hiki ambacho mwaka unaelekea kuisha ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga. 

Zoezi liliendeshwa kati ya tarehe 15 - 17 Disemba, katika jengo jipya la hospitali ya wazazi na watoto la CCBRT,na mamia ya wakazi wa Dar es salaam walijitokeza kwa wingi  kuchangia damu na kuokoa maisha ili kushughulikia tatizo la upungufu wa damu salama katika kipindi cha sikukuu. 

Kuanzia saa 2 asubuhi hadi 11 jioni kwa siku za Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi tarehe 15 hadi 17 Disemba, kampeni hii maalumu ya kuchangia damu ilifanyika kama sehemu ya mpango mkubwa wa mkoa chini ya mwavuli wa kampeni ya “Okoa maisha”, iliyozinduliwa Februari mwaka huu na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam. 

Kwa mkoa wa Dar es salaam, uhitaji wa damu ni mkubwa na matokeo ya ukosefu wa damu yanaweza kusababisha vifo: 

Kulingana na takwimu za Damu Salama, kwa wastani, lita 5000 za damu zinahitajika kwa mwezi, hata hivyo ni kiasi cha lita 3500 tu ndizo hukusanywa.
 Upungufu unakuwa na madhara makubwa wakati wa dharura hususan wakati wa uzazi.  Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa nchini Tanzania, wanawake 432 katika kila 100,000 wanaojifungua kila mwaka hufariki wakati wa uzazi, na asilimia 80 ya vifo hivi husababishwa na kutoka kwa damu nyingi (post-partum haemorrhage). 

Kampeni maalum za kukusanya damu kama Okoa Maisha zinakusudia kuhakikisha upungufu huo unatoweka na kwamba wakati wa dharura, damu salama inapatikana katika vituo vya afya na hospitali. Kwa kuwa damu inaweza kutunzwa kwa siku 35 tu, jitihada za kukusanya damu hufanyika kila wakati kwa mwaka mzima. 

Watu waliojitolea kutoa damu wanaombwa kujitolea mara kwa mara angalau mara mbili kwa mwaka. Inategemewa kuwa mpango huu wa damu utapata watu wengi na kukuza tabia ya kujitolea damu na wakati huohuo kufuta mawazo na hofu iliyotanda kuhusu uchangiaji wa damu kupitia njia rafiki, ya uhakika na salama.

 Kwa sasa, kampeni hii ya kuchangia damu ni kiungo muhimu katika mpango mzima wa CCBRT wa Changia damu, Okoa maisha: CCBRT kuongoza mpango wa kujitolea damu msimu huu wa sikukuu kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga. 

Mpango huu uliendeshwa katika jengo jipya la wazazi na watoto la CCBRT – lililo katika ujenzi – ambalo litakuwa kama hospitali maalumu ya rufaa kwa akina mama na watoto ndani ya mpango wa rufaa uliopo katika mkoa wa Dar es salaam wakati wa ufunguzi wake mwaka 2018. 

  CCBRT wanahusika pia katika mpango wa kujenga uwezo katika vituo 23 vya afya ndani ya mkoa wa Dar es salaam. 

Kupitia mpango huu CCBRT inatoa mafunzo, vifaa, mahitaji na miundombinu ya kuboresha msingi wa afya ya uzazi na watoto wachanga ndani ya mkoa. 

Mkakati huu unawezeshwa na msaada unaotolewa na Vodafone Foundation kupitia ushirikiano wa serikali na sekta binafsi pamoja na USAID/PEPFAR Mchango zaidi wa kifedha katika program hii unatolewa na serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada (GAC) Akichangia, Dr Brenda D’Mello, mshauri wa masuala ya ufundi kwa kitengo cha Mradi ya kujenga uwezo - Afya ya Uzazi na Watoto wachanga alisema:

 “Huu ni wakati wenye shughuli nyingi katika mwaka, wakati watu wanasherehekea kwa namna mbalimbali sherehe za mwishoni mwa mwaka, hospitali ya CCBRT, kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama na wadau wengine, ujumbe wetu katika majira haya kwa wakazi wa Dar es salaam ni kujitolea kuchangia damu ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga. Damu ni uhai, na haiwezi kupatikana kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kuchangiwa na watu wengine, hivyo tafadhali tuungeni mkono siku ya Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi!” 
Akizindua kampeni hiyo Bi. Magreth Mhando (Mkurugenzi wa tiba maendeleo ya afya jinsia na watoto
***************************************************************
Kuhusu CCBRT Ilipoanzishwa mwaka 1994, Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) ilianzishwa kama mpango wa kijamii inayotafuta watu wenye mtoto wa jicho mkoani Dar es salaam. Tangu wakati huo, tumekuwa mtoaji huduma mkubwa nchini wa huduma kwa wenye hali ya chini nchini Tanzania. Sisi ni taasisi isiyo ya kiserekali (NGO) iliyoandikishwa nchini Tanzania ikiwa na kusudi la kuwawezesha watu wenye ulemavu na familia zao kuboresha kiwango cha maisha na kuhakikisha upatikanaji wa madawa na matibabu kwa watu wote. 

Ikiwa imejitoa kuzuia ulemavu kwa kila inavyowezekana, CCBRT pia inajihusisha kwa kiasi kikubwa na shughuli za afya ya uzazi na watoto wachanga (MNHC) CCBRT inawahudumia watu masikini zaidi katika jamii na inajaribu kuondoa, kwa kadri inavyowezekana, vizuizi na kuwaruhusu watu kupata matibabu. Tunabadilisha maisha na jamii ya watu wanaoishi katika umasikini uliokithiri nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.