Habari za Punde

GLOBAL EDUCATION LINK WAISAIDIA SERIKALI KUZALISHA RASILIMALI WATU WENYE UJUZI

 Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Taasisi ya Global Education Link imeisaidia Serikali kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi na elimu ya kutosha ili watumike katika kuinua viwanda na uchumi wa nchi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Abdulmaliki Mollel alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa maonesho ya kwanza ya viwanda Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo jijini humo.

Mollel amesema kuwa Tanzania imeamua kuwa nchi ya viwanda lakini bila kuwa na rasilimali watu wenye ujuzi na elimu ya kutosha kuhusu uzalishaji na uendelezaji wa viwanda hakutakuwa na maendeleo kwani maendeleo yoyote mzizi wake ni elimu na ujuzi.

“Kuna  baadhi ya masomo ambayo ni muhimu hayapatikani katika vyuo vya Tanzania na kama zinapatikana basi nafasi ni chache hivyo,taasisi hii ni kama daraja la kutengeneza rasilimali watu wenye ubora watakaoleta maendeleo ya nchi kupitia kusoma nchi za nje,”alisema Mollel.

Ameongeza kuwa ili nchi ipate maendeleo kwa haraka ni lazima isaidiwe na taasisi na mashirika binafsi na ndio maana taasisi hiyo imeamua kuisaidia Serikali kwa kuwarahisishia Watanzania kupata elimu nje ya nchi ambayo itasaidia Serikali kupunguza matumizi pamoja na kuzuia wataalamu wa nchi za nje kufanya kazi nchini.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa mpaka sasa chuo hicho kimeshatoa wanafunzi takribani 5400 ambao wengi wao wameshika nyazfa mbalimbali kwenye taasisi za Umma na Binafsi.

Aidha, taasisi hiyo ina mpango wa kuandaa programu za miezi 4 hadi 6 ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi  kwa kupitia elimu ya vitendo kwenye viwanda mbalimbali vilivyoko nchini India.

Taasisi hiyo imeanzishwa mnamo mwaka 2006 ikiwa na lengo la kurahisisha mchakato na kuwaondolea usumbufu wanafunzi wanaohitaji kwenda kusoma nje ya nchi pamoja na kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.