Habari za Punde

MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA UHURU WA TANZANIA BARA

Sanamu ya Askari ikiwa imezungushiwa mapambo ikiwa ni siku nane (8) kabla ya kufikia kilele cha Maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara itakayofanyika tarehe 09/12/2016 katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni; “Tuunge Mkono Jitihada za Kupingaji Rushwa, Ufisadi na Kuimarisha Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo Yetu”. PICHA NA: FRANK SHIJA - MAELEZO
**************************************
Frank Mvungi-Maelezo
Kuelekea Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara Serikali imepongezwa kwa Mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi chote tangu awamu ya kwanza hadi awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Daniel Chongolo wakati wa mahojiano maalum kuhusu maadhimisho ya miaka hamsini na tano ya Uhuru  yanayotarajiwa kufanyika   kitaifa tarehe 9 Desemba mwaka huu.

“Tumepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa huduma za jamii kama vile elimu,Afya,Maji,usafirishaji na miundo mbinu ukilinganisha na wakati tunapata Uhuru” Alisisitiza Chongolo.

Katika Sekta ya elimu Chongolo anabainisha kuwa Serikali katika awamu zote tangu awamu ya kwanza hadi sasa zimekuwa zikiweka kipamaumbele katika Sekta  hiyo hali iliyochangia kuongezeka kwa shule za msingi ,Sekondari na Vyuo Vikuu .

Akifafanua zaidi Chongolo ameongeza kuwa elimu bure ni miongoni mwa  dhamira ya Serikali  ya Awamu ya tano  ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuzidi kuendeleza azma ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kupamabana na maudui watatu ambao ni ujinga,maradhi na umasikini.

Akizungumzia kuhusu miundo mbinu ya barabara anabainisha Tanzania ya sasa ina tofauti kubwa na wakati Taifa lilipokuwa likipata  Uhuru ambapo barabara za lami na madaraja yalikuwa machache lakini hivi sasa Mikoa yote inafikika kwa urahisi.

Anaongeza kuwa sekta ya maji pia imeimarika ukilinganisha na wakati wa uhuru ambapo moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali ni mradi wa maji wa ziwa Victoria hadi shinyanga na mwingine ni ule wa upanuzi wa mitambo ya Ruvu juu na Ruvu Chini ambayo imeanza kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam.

Aidha Chongolo aliwaaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali za Taifa na miundo mbinu iliyopo kwa maslahi ya taifa kwa kuwafichua wale wote wanaokwaamisha au kuhujumu nia njema ya Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Sherehe za Uhuru huadhimishwa kila mwaka inapofika tarehe 9 mwezi Desemba ambapo mwaka huu Kitaifa zitafanyika Jijini Dar es salaam na Kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza  tangu achaguliwe mwaka mmpja uliopita.


Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Tuunge Mkono Jitihada za Kupinga Rushwa,Ufisadi na Kuimarisha Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo yetu.”

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.