Habari za Punde

MFUMUKO WA BEI WAONGEZEKA KUTOKA ASILIMIA 4.5 MWEZI OCTOBA HADI ASILIMIA 4.8 MWEZI NOVEMBA


 Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epharaim Kwesigabo akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi Novemba mwaka huu, kulia kwake ni Mtakwimu Bw. Muhidini Mtindo. 
Wanahabari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epharaim Kwesigabo (hayupo pichani) wakati akielezea hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi Novemba mwaka huu. Picha na Benjamin Sawe-Maelezo.
****************************************
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dar es Salaam
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Novemba 2016 umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.5 iliyokuwapo  mwezi Octoba, 2016 kutokana na kuongezeka  kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa bidhaa za vyakula zikiwemo ngano,mbogamboga, mtama,  na vinywaji baridi zimechangia kuongezeka  kwa mfumuko wa bei nchini.

“Bidhaa nyingine zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini ni Nishati , mafuta  na viatu huku akibainisha kuwa kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini zimeongeka na kufikia 104.32 kwa mwezi Novemba 2016 ikilinganishwa na 99.54 za mwezi Novemba  mwaka jana” Alisema Kwesigabo.

Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi ameeleza kuwa umeongezeka kwa asilimia 1.1 kwa mwezi Novemba ikilinganishwa na asilimia 0.1 ya mwezi Octoba kutokana na kuongezeka kwa Fahirisi ya baadhi ya bidhaa zikiwemo unga wa ngano, unga wa mihogo, unga wa mahindi, mtama, dagaa, mchele.


Aidha, alisema kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania hupima badiliko katika kununua bidhaa na huduma zilezile za mlaji ambazo shilingi ya Tanzania ingeweza kununua katika kipindi tofauti, ikiwa fahirisi za bei za Taifa zinaongezeka uwezo wa shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma hupungua.


Kwa upande wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Kwesigabo alisema  kuwa una mwelekeo unaofanana ambapo Kenya umeongezeka  na kufikia asilimia 6.68 mwezi Novemba kutoka 6.42 za mwezi Octoba huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 4.6 mwezi Novemba kutoka asilimia 4.5 za mwezi Octoba.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.