Habari za Punde

MIAKA 55 YA MAMA MARIA NYERERE AIPONGEZA SERIKALI KWA KUBORESHA SEKTA YA ELIMU

Mama Maria Nyerere akizungumza na Afisa Habari wa Idara ya Habari – MAELEZO katika mahojiano maalum kuhusu maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru nyumbani kwake Mikocheni leo Jijini Dar es Salaam. PICHA NA FRANK SHIJA – MAELEZO
****************************************************
Na Georgina Misama, MAELEZO- Dar es Salaam.
SERIKALI ya Awamu ya Tano imepongezwa kwa namna ambavyo imetoa kipaumbele katika Sekta ya elimu chini ya mpango wa elimu bure, na hivyo kuongeza nafasi na hadhi ya mwanamke katika jamii.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mke wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere wakati wa mahojiano maalum kuhusu maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru nyumbani kwake Mikocheni Jijini Dar es Salaam. 

“Elimu imebadili nafasi ya mwanamke katika jamii, tukiangalia wakati tunapata uhuru wanawake wengi walikuwa bado hawajui kusoma na kuandika,” alisema Mama Maria Nyerere
Mama Maria aliongeza kuwa wakati Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961 idadi ya wanawake walioshika nafasi za uongozi walikuwa wachache sana na hazikuwa nafasi kubwa jambo ambalo ni knyume na hivi sasa kwani kwa mara ya kwanza Tanzania ina Makamu wa Rais mwanamama, Mama Samia Suluhu.

Aliongeza kuwa pamoja na changamoto zilizopo, Serikali za awamu zote zimekuwa zikijitahidi kuhakikisha zinapiga hatua katika kukabiliana na adui ujinga.
Kwa mujibu wa Mama Maria alisema ni faraja kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutambua umuhimu wa watoto kwenda shule kwa kuamua kutoa elimu ya bila malipo ya Ada, kwani hiyo inasaidia kupunguza watoto wa mitaani.

“Elimu imeleta ukombozi watoto waliokuwa awaendi shule walikuwa wanajikuta wanaingia katika makundi ndipo unasikia Panya road, mbwa mwitu na mengine,” aliongeza Mama Maria.
Aidha alisema kuwa ili taifa liweze kupata maendeleo ni lazima kujiamini, kuthubutu na kutenda kama ambavyo sasa Serikali imeamini na kuonesha uthubutu katika farsafa ya Hapa Kazi Tu na Tanzania ya viwanda.

Mama Maria ametoa rai kwa wakinamama kushirikiana katika kuhakikisha wanavitunza viwanda vinavyojengwa ili vieweze kuwa chachu ya maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.