Habari za Punde

RAIS WA FIFA AAGIZA TIMU ZOTE DUNIANI KUOMBOLEZA KWA DUA KABLA YA MCHEZO

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni Infantino bado ameguswa na vifo vya wachezaji wa timu ya soka Chapecoense Real ya Brazil vilivyotokea Jumatatu.

Rais Infantino ameagiza timu zote duniani kuendeleza utaratibu wa kuwaombea dua kabla ya mchezo kwa mechi zote zinazopigwa mwishoni mwa juma hili kuanzia leo Ijumaa ambao Tanzania kutakuwa na mchezo wa Ligi ya Vijana katika vituo vya Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.

Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Brazil (CBF), Lucca Victorelli kutokana na vifo hivyo vilivyotokana na ajali iliyoua zaidi ya watu 76 kati ya 81 waliokuwa kwenye ndege moja.

Kwa upande wake, Rais Infantino ametuma waraka kwa kila Shirikisho au Chama cha Mpira wa Miguu Duniani akisema kwamba utamaduni wa kusimama kwa dakika moja uendelezwe kwa kila mchezo utakaochezwa kuanza leo Ijumaa hadi Jumatatu.

Ishara za maombolezo hayo, ziende sambamba na kufunga kitambaa cheusi mkononi ili kuwakumbuka wachezaji hao, wanahabari kadhalika abiria wengine ambao kwa pamoja walikuwa kwenye ajali hiyo iliyonusurisha watu watano tu.

Ndege hiyo iliyotumiewa na wacheaji hao wakiwamo abiria wengine ilikuwa ikisafiri Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana). Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa Jumatano Novemba 30, 2016 ambako Chapecoense Real ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya Brazil na awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye karibu na mji wa Medelin.

Wachezaji walionusurika wanatajwa kuwa ni Alan Ruschel, golikipa Danilo na Jackson Follmann na kwamba walipatiwa huduma ya kwanza katika hospitali iliyoko katika mji wa Le Ceja nchini Colombia.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.