Habari za Punde

RAIS WA ZANZIBAR DKT SHEIN ATEMBELEA MAJENGO MAPYA YA ZIMAMOTO UWANJA WA NDEGE

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Kamishana wa Kikoso cha Zima Moto Zanzibar Abdalla Malimosi wakati alipokuwa akiaangalia picha za magari mapya ya kikosi hicho yanayotarajiwa kuwasili hivi karibuni,wakati alipotembelea ujenzi wa majengo mapya ya kikkosi hicho leo huko katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Wilaya ya Magharibi "A"Unguja
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar na Uongozi wa Kikosi cha Zima Moto na Uokozi, wakati alipofika kutembelea ujenzi wa majengo mapya ya kikosi hicho leo. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Jengo hili kama linavyoonekana baada ya kumalizika Ujenzi wake ambapo Kikosi cha Zimamoto na Uokozi itakuwa ni Ofisi ya Kikosi hicho.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (wa pili kushoto) akiangalia baadhi ya Vyumba vya Ofisi mpya ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume huko Kisauni Wilaya ya Magharibi "A"Unguja leo,(wa pili kulia)Kamishna wa Kikosi hicho Abdalla Malimosi na SACF Simai Haji Simai
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Abdalla Malimosi wakati alipotembelea kituo kidogo kinachofayiwa matengenezo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume akiwa katika ziara maalum leo,(kushoto) Naibu Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji Mhe,Mohamed Ahmed Salum,(wa pili kushoto) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe,Haji Omar Kheri. Picha na Ikulu.
**********************************************
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuridhika kwake na ujenzi wa ofisi za Zimamoto alizoagiza kujengwa ndani ya miezi miwili katika ziara yake aliyoifanya Oktoba 4 mwaka huu huko katika eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. 
Dk. Shein alitoa agizo hilo mara baada ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Zimamoto huko katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, mnamo Oktoba 4 mwaka huu ambapo ujenzi huo ulionekana kusuasua kwa muda mrefu lakini leo ameeleza kuridhika na ujenzi huo. 
Katika maelezo yake mara baada ya kukagua jengo la ofisi hizo Dk. Shein alisema kuwa alipongeza hatua za ujenzi zilizofikiwa na kupongeza kwa kazi nzuri iliyofanywa licha ya kuwa imo katika hatua za ukingoni kumaliza.

“Niliahidi miezi miliwi iliyopita kuwa nitakuja kuangalia ujenzi wa jingo hili lakini leo nimekuja kwa furaha, kazi nzuri imefanyika na nimeridhika kwa kuona pamoja na maelezo mliyonipa ya asilimia ya hatua za ujenzi, hongereni sana”,alisema Dk. Shein. 
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ni matumaini yake makubwa kutokana na kasi ya ujenzi inavyokwenda si zaidi ya wiki mbili zijazo kazi hiyo itakuwa imemaliza kabisa. 
Dk. Shein alipongeza kwa mashirikiano makubwa yaliofanyika kati ya taasisi husika na kupelekea ujenzi huo kukamilika kwa wakati muwafaka kutokana na mipango mizuri waliyoifanya na kuitekeleza.

Alisema kuwa mradi wa ujenzi huo umejenga uzoefu mkubwa kwa taasisi husika katika masuala mazima ya kujenga kwa kujipangia taratibu zao wenyewe za ujenzi kama alivyoagiza ambazo zinaepusha matumizi makubwa ya fedha. 
Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na ujenzi huo pamoja na sehemu muhimu zilizomo ndaji ya jingo hilo ambazo zinatoa fursa nzuri kwa wafanyakazi wa Zimamoto kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi kwani mambo yote yanayohitajika yamo ndani ya jengo hilo. 
Alisema kuwa ameridhishwa na ofisi zilizomo ndani ya jingo hilo, vyumba vya wafanyakazi wa kike na kiume, vyoo pamoja na stoo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya shughuli za zimamoto. 
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kufanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja na kuepuka mivutano ambayo haina tija katika utendaji wa kazi.

Pia, Dk. Shein alieleza matarajio ya ujio wa gari nne za zimamoto zinazotarajiwa kuwasili hivi karibuni ambazo mbili zimenunuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mbili zimenunuliwa kutokana na mkopo wa fedha za Benki ya Dunia ambazo zinatoka nchini Afrika ya Kusini na Dubai. 

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kuwathamini watendaji wake katika sekta za umma ambapo tayari katika uongozi wake wafanyakazi wa sekta za umma wameshapandishiwa mishahara mara tatu mnamo mwaka 2011,2013 na 2015. 

Hata hivyo Dk. Shein alisema kuwa Serikali imo katika taratibu za kuangalia upandishaji wa madaraja kwa wafanyakazi hao wa sekta za umma kwa ngazi tofauti huku akisisitiza azma yake kwa vikosi vya SMZ kupata maslahi yanayolingana na yale ya vikosi vya SMT. 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alimueleza Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa watendaji wa taasisi zote husika kwa kazi hiyo nzuri iliyofanywa na kutekeleza agizo lililotolewa na Rais kwa ufanisi mkubwa na hatua iliyobaki na ni kitaalamu. 

Kamishna wa Idara ya Zimamoto Zanzibar Ali Abdalla Malimosi nae alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo na kuwapongeza mafundi wa ujenzi huo huku akiwaahidi kuwapandisha daraja mafundi hao kutoka Idarani kwake waliojenga jengo hilo.

Mapema akiwa katika ukumbi wa wageni maalum wa uwanja wa ndege mkongwe wa Abeid Amani Karume, Dk. Shein alipata maelezo ya ukamilishaji wa ofisi hizo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Abdulghani Himid Msoma ambapo alieleza kuwa ujenzi huo umefikia kiwango kisichopungua asilimia 92 ya kazi zote.

Musoma akiyataja maeneo matano yaliolengwa katika kutekeleza kazi hiyo ni pamoja na ukarabati mkubwa wa banda kongwe na kuligeuza kuwa jengo kubwa la kituo cha Zimamoto kilichotimia kwa mujibu wa mahitaji kamili ya kazi za Zimamoto. 

Aidha, ukarabati wa ofisi ndogo kwa ajili ya huduma za utawala, uimarishaji wa kituo kilichopo hivi sasa kwa kujenga kutumika kuwa ‘satellite post’, kusafisha bwawa na kukamilisha miundombinu ya maji na kuweka miundombinu ya kudumu ya umeme. 

Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeleta mafanikio makubwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, kwa vile uwanja umepata kituo cha Zimamoto cha kudumu kinacholingana na hadhi ya uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Kwa maelezo ya Mwenyekiti huyo, kazi hiyo ya ujenzi huo inatarajiwa kugharimu Tsh. Milioni 335 ambapo hadi sasa asilimia 92 zimetumika ambazo ni milioni 310 fedha zote hizo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar.

Dk. Shein alimalizia ziara yake hiyo kwa kuangalia kituo kidogo cha Zimamoto ambacho kinatarajiwa kuwepo ndani ya eneo la uwanja wa ndege kama ilivyo kwa viwanja vyengine va kimataifa ambacho kinaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.