Habari za Punde

TFDA YATOA WITO KWA WAZALISHAJI KUJIUNGA KATIKA VIKUNDI.

 Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bibi. Gaudencia Simwanza akiwasilisha mada wakati wa semina maalum kwa wajasiriamali wanawake iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuelekea kilele cha maonesho ya viwanda vya Tanzania jana jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bibi. Gaudencia Simwanza akigawa vipeperushi wakati wa semina maalum kwa wajasiriamali wanawake iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuelekea kilele cha maonesho ya viwanda vya Tanzania jana jijini Dar es Salaam. Picha na Frank Shija – MAELEZO.
*************************************************
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imetoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba kujiunga katika vikundi ili waweze kupata mafunzo kwa urahisi pamoja na kusaidiana kiuchumi.

Wito huo umetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Mamlaka hiyo, Gaudencia Simwanza wakati akitoa mafunzo katika semina ya wakina mama wajasiriamali iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na kufanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo jijini humo.

Gaudencia amesema kuwa ni lazima kuchunguza kwa makini bidhaa mbalimbali zinazohusisha afya ya binadamu  kwa ajili ya kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa hizo ili zisiweze kumdhuru mtumiaji hivyo, mamlaka hiyo haijawekwa kwa bahati mbaya bali ina madhumuni thabiti ya kulinda afya ya watumiaji wa bidhaa hizo.

“ili kuhakikisha bidhaa hizo ni salama kwa afya ya mtumiaji ni lazima kuhakikisha tunatoa elimu na mafunzo kwa wazalishaji  ili waweze kuzalisha kulingana na utaratibu mzuri uliowekwa ndio maana tunawashauri wajiunge kwenye vikundi ili iwe rahisi kupata elimu pamoja na kupata nafasi kubadilishana mawazo yanayohusu uzalishaji wa bidhaa zao,” alisema Bi Gaudencia.

Afisa Mahusiano huyo ameongeza kuwa, kwa kuwa sifa ya kwanza ya kusajiliwa katika Mamlaka hiyo ni kuwa na jengo la uhakika na salama kwa ajili ya kuzalishia bidhaa hizo, hivyo uundaji wa vikundi vya pamoja utasaidia wazalishaji kutafuta fedha kwa pamoja kwa ajili ya kupata jengo kwani wazalishaji wengi wamekua wakilalamika kukosa fedha kwa ajili ya jengo la kufanyia shughuli hizo.

Amefafanua kuwa mbali na vikundi hivyo, Mamlaka hiyo imekua ikitoa elimu kwa wajasiliamali mbalimbali kupitia ofisi za za kanda zilizopo katika Mikoa 7 nchini ikiwemo ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Mashariki, Magharibi, Kaskazini, Kusini na Kanda ya Kati.

Amewasisitiza wajasiriamali wote wanaozalisha bidhaa zinazohusisha afya ya binadamu kusajili majengo yao pamoja na kusajili bidhaa zao ili kupata Hati ya Usajili wa Jengo pamoja na kibali cha kutengenezea bidhaa hizo mara baada ya kukamilisha taratibu zote zilizoainishwa kisheria.

TFDA ni taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyoundwa kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha bidhaa zinazohusika na afya ya mtumiaji zinatengenezwa katika hali ya usafi na usalama.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.