Habari za Punde

TRA YATOA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI JUU YA ULIPAJI KODI.

Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA Idara ya Kodi za Ndani Bw. George Haule akitoa mada wakati wa semina ya wajasiriamali wanawake iliyofanyika wakati wa maonesho ya viwanda vya Tanzania jana jijini Dar es Salaam.
*********************************************************
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu kodi ili waweze kufahamu aina na madaraja ya kodi pamoja na umuhimu wa ulipaji kodi.

Mafunzo hayo yametolewa jana na Afisa wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, George Haule katika semina ya wakina mama wajasiriamali iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na kufanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo jijini humo.

Haule amesema kuwa katika uanzishaji wa biashara ya aina yoyote jambo la kwanza na muhimu ni kujisajili katika mamlaka hiyo na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN - Number) itakayomuwezesha mfanyabiashara au mjasiriamali kuwa na biashara halali ambayo inalipiwa kodi kulingana na mauzo au faida ya biashara husika.

”Tanzania ni nchi yetu na sisi Watanzania ndio tuna jukumu la kuitunza nchi hii, njia rahisi ya kuitunza nchi ni kulipa kodi stahiki ili kuinua pato la taifa kwa sababu kodi ndio chanzo kikubwa cha mapato ya nchi,”alisema Haule.

Haule ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inatumia mfumo endelevu wa ulipaji kodi kwa maana ya kila mfanyabiashara mdogo mwenye mauzo yasiyozidi 20,000,000 kulipa kodi ya mwaka kulingana na mauzo yake na mwenye mauzo yatakayozidi kiasi hicho cha fedha kulipa kodi ya mwaka kulingana na faida anayoipata katika biashara husika.

Amefafanua kuwa wafanyabiashara wadogo wamegawanyika katika makundi matano ambapo wenye mauzo ya kuanzia shilingi 1 hadi 4,000,000 kwa mwaka hawalipi kodi yoyote, wenye mauzo kuanzia 4,000,000 hadi 7,500,000 wanalipa kodi ya shilingi 150,000 kwa mwaka, wenye mauzo kuanzia 7,500,000 hadi 11,050,000 wanalipa shilingi 318,000 kwa mwaka, wenye mauzo kuanzia 11,050,000 hadi 16,000,000 wanalipa shilingi 546,000 kwa mwaka na wenye mauzo kuanzia 16,000,000 hadi 20,000,000 wanalipa shilingi 862,000.

Ameendelea kufafanua kuwa mfanyabiashara mwenye mauzo ya zaidi ya 20,000,000 sheria itamtaka aandae mahesabu ya mauzo yake ili aweze kulipa kodi kulingana na faida anayoipata kwa mwaka mmoja.


Amewaasa wafanyabiashara kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya ufanyaji wa biashara nchini ili kwa pamoja tushirikiane katika kuijenga Tanzania yenye maendeleo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.