Habari za Punde

WAKULIMA WATAKIWA KUTUMIA PEMBEJEO ASILIA KUKUZA KILIMO HAI

             Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Wataalamu wa kilimo wamewataka wakulima mkoani Morogoro kutumia pembejeo za asili ili kuepuka kemikali zenye sumu zinazotokana na pembejeo za viwandani ambazo zinaathiri usalama wa chakula. 
Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini Morogoro katika mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania wakishirikiana na Shirika la TOAM kupitia Mradi wa Masuala ya Kilimo Unaozingatia Utunzaji wa Mazingira.
Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa Shirika linalohamasisha utunzaji wa bionuwai ya kilimo Tanzania (TABIO), Abdallah Ramadhani amesema kuwa  lengo la mafunzo hayo ni kuweza kutoa elimu juu ya umuhimu na matumizi sahihi ya pembejeo za asili kwa ajili ya kukuza na kuendeleza kilimo hai nchini hasa kwa kuangalia njia zinazotumika kutengeza mbolea na madawa ya asili ili kuhakikisha wakulima nchini wanaachana na matumizi ya viuatilifu vya viwandani ambavyo vina kemikali.

“Viuatilifu vyenye kemikali za kuua wadudu waharibifu zenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 30 humwagwa kwa makusudi katika mazingira ya dunia kila mwaka, sehemu kubwa ya viuatilifu hivyo ni vile vyenye sumu kali ambazo zina athari za moja kwa moja kwa afya ya binadamu, wanyama pori pamoja na vyanzo vya chakula ndio maana tunawashauri wakulima kuacha kutumia pembejeo za aina hiyo”,alisema Ramadhani.
Akibainisha baadhi ya madhara yatokanayo na viutalifu hivyo toka viwandani, Ramadhani amesema kuwa pamoja na kuathiri afya na usalama wa viumbe hai, viuatilifu hivyo vinatumiwa bila ya kuwa na vifaa kinga pia huchafua mzingira na hata kuua viumbe wengine wasiokusudiwa.
Ameongeza kuwa, baadhi ya viuatilifu hivyo vina athari za muda mrefu kwa binadamu ikiwemo matatizo ya uzazi, dosari za kuzaliwa, kuvuruga mfumo wa homoni na kuharibu mfumo wa kinga.
Kwa upande wake Meneja wa Viwango na Ubora toka Kampuni ya Guavay inayotengeza mbolea aina ya HAKIKA Organic Fertilizer, Latifa Mafumbi amewasihi wakulima kuendelea kutumia pembejeo za asili kwa kuwa hazina madhara kuanzia kwa mtengenezaji, ardhi, mimea, viumbe, wadudu wanaorutubisha ardhi pamoja na mlaji. 
Amesema kuwa kama mtaalamu, kwa sasa anaendelea kufanya uchunguzi kwenye zao la nyanya ili kubaini tofauti iliyopo kwenye zao hilo kama atatumia mbolea ya kiwandani yenye kemikali na mbolea iliyotengenezwa kiasili kwani tafiti nyingi za awali zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea za asili hutoa mazao bora.
Naye mkulima mshiriki, Pius Paulini amebainisha kuwa kilimo hai kinachotokana na matumizi ya pembejeo za asili (mbolea na madawa) kimekuwa kikiongeza rutuba kwenye ardhi hivyo kuwasaidia wakulima kulima kwenye eneo moja kwa kipindi kirefu pasipo kuhamahama. 
Amefafanua kuwa mimea hustahimili mabadiliko ya tabianchi tofauti na viuatilifu vya viwandani vilivyojaa kemikali yenye sumu na kuchangia kwa asilimia kubwa kufifisha ubora wa ardhi na hata kuua wadudu ambao wanasaidia kurutubisha mimea shambani.
PELUM ni shirika linalohamasisha utunzaji na matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuepuka athari kwenye kilimo na shirika la TOAM ni shirikalinalohamasisha Kilimo Hai Tanzania.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.