Habari za Punde

AZAM FEDERATION CUP KUENDELEA KURINDIMA KESHO

Baada kupatikana timu nne kutoka Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) katika michuano ya Kombe la Shirikisho ya Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), mapambano ya kuwania taji hilo, yanatarajiwa kuendelea kesho Januari 12, 2017 kwenye viwanja tofauti hapa nchini kwa kuzihusisha timu za Ligi Daraja la Pili (SDL).

Timu nne zilizofanya vema hatua ya mwanzo iliyoshirikisha timu 22 za RCL ni Jangwani ya Rukwa ambayo kesho Januari 12, mwaka huu itacheza na wenzao wa Stand Bagamoyo kwenye Uwanja wa Mandela ulioko Msata mkoani Pwani. Mchezo uliopewa jina la Namba 41.

Pia Kabela City ya Shinyanga itacheza na Murusagamba ya Kagera kwenye Uwanja wa Kahama huko mkoani Shinyanga katika mchezo Na. 42, huku ratiba hiyo ikiendelea kwa timu za Daraja la Pili ambako Green Warriors ya Pwani kucheza na Cosmopolitan ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Mabatini uliko Mlandizi mkoani Pwani; mchezo Na 43.

Mchezo Na. 44 utakutanisha timu za Changanyikeni ya Dar es Salaam na Burkina Faso ya Morogoro kwenye Uwanja wa Karume jijini wakati Mawezi ya Morogoro itaikaribisha Oljoro ya Arusha kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kwenye mchezo Na. 45 huku Madini wakiwa wenyeji wa Mirambo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha katika mchezo Na. 46.

Namungo FC ya Lindi itakuwa mgeni wa The Mighty Elephant ya Songea kwenye dimba la Majimaji katika mchezo Na. 47 wakati Mashujaa ya Kigoma itaikaribisha Kitayosa ya Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma kwenye mchezo Na. 48.

Mshindi wa mchezo Na. 41 atacheza na mshindi wa mchezo Na. 42; Mshindi wa mchezo Na. 43 atacheza na mshindi wa mchezo Na. 44; Mshindi wa mchezo Na. 45 atacheza na mshindi wa mchezo Na. 46 na Mshindi wa mchezo Na. 47 atacheza na mshindi wa mchezo Na. 48. Mechi hizo zote zitafanyika Januari 15, 2017.

Hatua itakayofuata ni itaanza kwa kuzishirikisha timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambako KMC ya Kinondoni itacheza na Kiluvya United ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam Jumamosi Januari 14, mwaka huu.

Hatua hiyo itafuatia pia kwa siku ya Januari 15, 2017 na Januari 16, mwaka huu kwenye viwanja tofauti.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.