Habari za Punde

BAADA YA AJALI YA JANA HATIMAYE NJIA YA RELI KATI YA DAR ES SALAAM NA RUVU YAFUNGULIWA

 KAMPUNI YA RELI TANZANIA(TRL)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI –PRESS RELEASE
HATIMAYE NJIA YA RELI KATI YA DAR ES SALAAM NA RUVU YAFUNGULIWA !

Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umetoa taarifa kuwa kuanzia saa 9 alasiri  leo Januari 30, 2017 njia ya reli kati ya Kituo Kikuu cha  Dar es salaam na Ruvu imefunguliwa rasmi kwa shughuli za uendeshaji wa reli.

Taarifa hiyo imesema kuwa kazi ya ufunguaji njia imewezekana baada ya Wahandisi na  Mafundi wa reli kuyaondoa Mabehewa yaliopata ajali l kutoka relini  na pia kuikarabati sehemu iliyo haribika . Kazi hiyo imefanyika kuanzia usiku wa Januari 29, 2017  hadi mchana wa Januari 30, 2017.

Aidha treni ya abiria iliyoahirisha safari  ya kuondoka kwenda bara jana imeondoka leo  saa 9:05 alasiri kutoka kituo kikuu cha Dar es Salaam kwenda bara..

Wakati huo huo imefahamika kuwa msafiri mmoja aliyetambulikana kama Nd Basekena O. Bango kutoka Bujumbura Burundi akiwa  anasafiri kutoka Kigoma amelazwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani wa Pwani kwa ajili ya matibabu zaidi. Aligunduliwa kuwa amechanika mguu wake wa kulia hivyo basi kuhitaji kushonwa mguu wake huo.

Taarifa kutoka Muhimbili zinaeleza kulazwa kwa majeruhi wawili waliopokelewa hospitalini hapo usiku wa Januari 29, 2017. Majeruhi wamefamika kuwa ni Nd. Stephania Mbona (46) kutoka Kigoma alikuwa amekuja Muhimbili kuendelea na matibabu ya ugonjwa wa tumbo, hata hivyo alitibiwa majeraha ya kawaida na anaendelea kulazwa kwa ajili ya  matibabu ya ugonjwa wake wa tumbo.

Mgonjwa wa pili Nd Alice Jovin (37) mkazi wa Salasala  Dar es Salaam alikuwa anatoka Kigoma kuja Dar es Salaam amepata majeraha ya kawadia ametibiwa na alitarajiwa kuruhusiwa leo asubuhi.

Kuhusu idadi ya wasafiri treni ya Deluxe yenye uwezo wa kusafirisha abiria zaidi ya 1000 wakati inapata ajali ilikuwa na abiria 480.

Aidha imefahamika kuwa ili kufahamika hasara na sababu za ajali hiyo taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguzi wa Kamati maalum  inayoundwa  kwa mujibu  wa sheria, taratibu  na kanuni za uendeshaji reli za kimataifa. Taarifa hiyo itatolewa baada ya wiki mbili.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano:
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
Januari 30, 2017
DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.