Habari za Punde

BILIONI 13.1 KUTUMIKA KUGHARIMIA MIRADI YA MAENDELEO SINGIDAMkurugenzi Bravo Kizito Lyampembile (wa kwanza kushoto) na Meya Manispaa ya Singida, Chima Gwae (katikati) wakitiliana saini mkataba wa mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 5.75 za mjini hapa kwa kiwango cha lami,na mwakilishi wa kampuni ya China Henan Internatioanl Co operation Ltd ya jijini Dar es salaam, Bi. Zephyr Liu. Ujenzi huo utagharimu zaidi ya shilingi 13.1 bilioni ambazo zimetolewa na benki ya dunia.
******************************************
Na Nathaniel Limu Singida.
Halmashauri ya manispaa ya Singida inatarajia kutumia zaidi ya shilingi 13.1 bilioni, kwa ajili ya kugharamia miradi mitatu ya uimarishaji miji (ULGSP) inayogharamia na benki ya dunia.
Hayo yamesemwa juzi na Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyapembile, wakati akizungumzia kwenye hafla ya sherehe ya kusaini mkataba baina ya manispaa, washauri na mkandarasi atakayetekeleza miradi hiyo.
Amesema wamefikia hatua hiyo ya kusaini mkataba baada ya taratibu zote za kisheria za manunuzi kukamilika na kuongeza kuwa miradi hiyo ni ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 5.75 kwa kiwango cha lami.
“Barabara hizo ni pamoja na ile inayoanzia kituo cha mafuta Namfua hadi ofisi ya Mamlaka ya mapato (TRA) ambayo itapanuliwa na kuwa mbili (double road). Nyingine ni ile inayoanzia ofisi za TRA hadi makazi ya askofu wa kanisa la katoliki (barabara ya Kinyeto)”, ameongeza.
Lyampembile amesema taratibu za manunuzi katika mkataba huu zilianza mwezi Mei mwaka jana na kukamilika Januari mwaka huu ambapo ujenzi huo utagharimu zaidi ya shilingi 12.4 bilioni.

“Leo hii manispaa ya Singida itatiliana saini mkataba namba LGA/115/SMC/2016/2017 /W/NO.1 na kampuni ya China Henan International Co-operation Group Co.LTD (CHICO) ya jijini Dar-es-salaam. Ujenzi huo utakamilika baada ya miezi 12”, alifafanua zaidi.
Amesema CHICO atasimamiwa na kampuni ya Luptan Consultants Ltd ya jijini Dar-es-salaam kwa gharama ya shilingi 648.3 milioni na itakamilika baada ya miezi 15. Mkataba wa mradi huo ni LGA/115/SWMC/2016/2017/C/No.02.
“Vile vile tutatekeleza mradi mwingine wa uandaaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa mansipaa yetu ya Singida.Mradi huu wenye mkataba LGA/115/SMC/2016/2017/C/No.03 una thamani ya zaidi ya shilingi 55.9 milioni.Mradi huu utatekelezwa na mshauri mwelekezi chuo cha mipango Dodoma, Titus Mwageni”,alisema.
Sherehe hiyo ya utiaji saini mikataba hiyo,zilihudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Singida Elias Tarimo na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi.
Dk.Nchimbi Alitumia fursa hiyo kuyaomba mashirika ya TANESCO,TTCL na mamlaka ya maji (SUWASA) kutoa ushirikiano na mkandarasi,ili miundo mbinu yao isikwamishe utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao utakapokamilika,utabadilisha madhari ya mji wa Singida.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.