Habari za Punde

DKT. MGWATU AWATAKA WATENDAJI TEMESA KUEPUKA WAZABUNI WANAOUZA VIPURI NA VILAINISHI KWA BEI ISIYO YA SOKO.

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (aliesimama) akifungua mafunzo elekezi juu ya tozo za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo kwa watumishi wa TEMESA kutoka mikoa 19.  Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Uzalishaji na Matengenezo Mhandisi Sylvester Semfukwe na kulia ni Meneja wa TEMESA Dodoma. Mafunzo hayo ya siku 5 yanafanyika Mkoani Dodoma katika ukumbi wa TBA.
Washiriki wa mafunzo elekezi juu ya tozo za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo yanayofanyika Mkoani Dodoma katika ukumbi wa TBA wakisikiliza hotuba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (hayupo pichani). Mafunzo hayo ya siku tano yanashirikisha watumishi wa TEMESA kutoka mikoa 19.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi juu ya tozo za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo yanayofanyika mkoani Dodoma katika ukumbi wa TBA wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (alieketi katikati) baada ya ufunguzi. Mafunzo hayo ya siku tano yanashirikisha watumishi wa TEMESA kutoka mikoa 19.
Mameneja kutoka mikoa 19 yenye vituo vya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (alieketi katikati) baada ya ufunguzi wa mafunzo elekezi juu ya tozo za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo yanayoendelea mkoani Dodoma katika ukumbi wa TBA
 Picha zote na Theresia Mwami, TEMESA.
****************************************************

Na Theresia Mwami, TEMESA.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu leo amefungua mafunzo elekezi kwa mameneja wa mikoa na vituo vya TEMESA juu ya tozo za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo pamoja na uaandaji wa taarifa za uzalishaji za mwezi kwa watumishi wa TEMESA kutoka katika mikoa na vituo mbali mbali vilivyopo nchini.
Katika hotuba yake Dkt. Mgwatu amewataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanashiriki mafunzo hayo kwa umakini mkubwa ili kuleta mabadiliko chanya kwa TEMESA na kuondoa kero mbalimbali zilizopo sasa, ikiwemo kero ya gharama kubwa za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya serikali na kuwataka watumishi hao kuondokana na wazabuni wanaouza vipuri na vilainishi vya magari kwa bei ghali isiyo ya soko.
“Mafunzo haya ni gharama na kwa hiyo haitakuwa jambo jema tukarudi katika vituo vyetu na kuendeleza mambo yale yale kwa mazoea. Tutakuwa hatujatenda haki kwa wananchi na kwa taifa kwa ujumla. Niwe mkweli kuwa nitachukua hatua kali pale nitakapoona mkoa au kituo hakifanyi vyema katika utendaji kazi wake” alisema Dr. Mgwatu.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo Mhandisi Sylvester Semfukwe amesema kuwa idara yake imeandaa mada mbali mbali kwa ajili ya mafunzo hayo zikiwemo: Tozo ya matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo kwa kuzingatia muda halisi wa matengenezo, Mfumo mpya wa kuandaa taarifa za uzalishaji za kila mwezi, Namna ya kubaini vipuri bandia kwa njia ya kielektroniki, Masuala ya masoko na huduma kwa mteja pamoja na mwongozo wa uwandaaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18.
Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza jana katika Ukumbi wa TBA mkoani Dodoma, yanashirikisha jumla ya mikoa 19 yenye vituo vya TEMESA, yanatarajia kukamilika Ijumaa tarehe 20/01/2017. Aidha mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo kama hayo yaliyofanyika mwezi Desemba, 2016 mkoani Dar es Salaam na yalishirikisha mikoa sita.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.